Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dk Angelina Mabula akizungumza kwenye mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi na mapambano dhidi ya ukatili kwa Wazee
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 na mapambano dhidi ya ukatili kwa Wazee
Baadhi ya wazee walioshiriki kwenye mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi na mapambano dhidi ya ukatili kwa Wazee wakiwa kwenye maombi
***************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wazee kutoka Kata 19 zilizoko katika Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza wamepewa mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agositi 23 mwaka huu na mapambano dhidi ya ukatili.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Alhamisi Julai 14,2022 katika ukumbi wa Monarch Hotel uliopo Jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala, amewaomba wazee kupitia elimu watakayoipata wakawe walimu katika Jamii kwa kuwaelimisha umuhimu wa sensa ili muda utakapofika kila mmoja aweze kushiriki kikamilifu.
Akizungumzia ukatili Masala amesema kuwa jamii inapaswa kuwa na malezi mazuri kuanzia kwenye ngazi ya familia ili kuweza kutengeneza kizazi chenye maadili na chenye hofu ya Mungu hali itakayosaidia kupunguza au kumaliza kabisa vitendo vya ukatili vinavyosababisha kupoteza ndoto za watu.
Kwa upande wake Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dk. Angelina Mabula amesema kuwa wazee wanamakundi makubwa ya watu hivyo anaimani elimu hiyo itafika kikamilifu kwenye jamii.
Naye Mratibu wa sensa Mkoa wa Mwanza Goodluck Lyimo,amesema zoezi la sensa ya watu na makazi ni la muhimu sana kwani linaipatia Serikali takwimu za msingi zinazotumika kutunga sera, kupanga mipango ya maendeleo pamoja na kufatilia utekelezaji wake.
Transisi Balizukwa (67) ni mshiriki wa mafunzo hayo amesema vijana wengi wanapuuza kuhesabiwa hivyo kupitia elimu aliyoipata atakwenda kuwaelimisha vijana ili waweze kuelewa umuhimu wa sensa, hatuhesabiwi kwaajili ya biashara tunahesabiwa ili tuweze kupata maendeleo na kupata huduma mbalimbali kwa urahisi.
“Mimi binafsi ninamtoto wangu anaumwa ugonjwa wa kupooza hivyo zoezi la sensa litakapofika watamhesabu na kumuingiza kwenye takwimu hali itakayosaidia kupewa msaada”, amesema Balizukwa
Amina Said,Mkazi wa Buzuruga Kasikazini amesema kupitia elimu aliyoipata atakwenda kuhamasisha kaya yake na kaya jirani ili waweze kutambua umuhimu wa kuhesabiwa.
Amesema atahamasisha kaya ambazo zinawatu wenye ulemavu kuwatoa ili waweze kuhesabiwa hali itakayoisaidia Serikali kupata idadi kamili ya walemavu waliopo katika sehemu husika.