Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema wakati Watanzania wakifikisha miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi nchini, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Omari Ali Juma pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad wametoa mchango mkubwa kuufanikisha.
Aidha, kimesema viongozi hao wameacha mafunzo muhimu kwa Watanzania kwani walikuwa mstaribwa mbele katika kusimamia uzalendo, uvumilivu na kuamini katika maridhiano kwa lengo la kuhakikisha nchi inakuwa salama.
Akizungumza kwa nyakati tofauti alipozuru makabuli ya viongozi hao akianza na kaburi la Dk. Omari lililopo ChakeChake Pemba na baadae kaburi la Maalim Seif lilipo Kijiji cha Mnyali Shehi aua Mtambwe Kaskazini kisiwani humo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema viongozi hao wametoa mchango mkubwa katika medani za siasa nchini.
Akiwa katika kaburi la hayati Dk. Omari, Shaka alisema imetimia miaka 21 sasa tangu kiongozi huyo alipoitwa na Mwenyezi Mungu na akaitika. “Miaka 21 ya kutokuwepo kwa Dk. Omari Ali Juma imekuwa na funzo kubwa kama taif, wote tunakumbuka katika uhai wake alikuwa kiongozi ambaye ni nguzo iliyotegemewa ndani ya Zanzibar lakini na Tanzania.
” Dk. Omari ni kiongozi ambaye kwa nyakati zote hakuacha kuishi kwenye uzalendo, hakuacha kuishi kwenye uanamapinduzi halisia, lakini Dk. Omar alibeba dhana ya ukombozi wa visiwa vya Unguja na Pemba na uhuru wa Tanzania na kwa nyakati zote alizoaminiwa katika nafasi zote alitimiza wajibu wake kwa weledi, alitimiza wajibu wake kwa uthubitu, lakini alitimiza wajibu wake kwa uaminifu mkubwa,” alisema Shaka.
Aliongeza kuwa jambo ambalo ameliacha kama darasa kwa wananchi hususan viongozi katika umri ambao Mungu atawajaalia kuishi duniani.
Aidha, alisema wakati Watanzania wakimwombea Dk. Omari nchi inatimiza miaka 30 tangu kuasisiwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, hivyo huwezi kuzungumzia miaka 30 ya demokrasia ndani ya Tanzia bila ya kuzungumzia mchango wake katika kuhuisha na kudumisha demokrasia.
“Dk. Omar Ali Juma alikuwa mwanasiasa nguli aliyetoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambaye alikibeba Chama hiki kwenye mabega yake tangu akiwa ASP hatimaye Chama Cha Mapinduzi, nyakati zote alitimiza wajibu wake wa kukipigania, kukisimamia na kuhakikisha kwamba Chama kinakuwa mkombozi kwa wana CCM wa Unguja na Pemba,” alisema.
Alisema Dk. Omari hatasahaulika katika kurasa za kumbukumbuku hasa kisiwani Pemba kwani alifanya kazi kubwa ya kuleta mageuzi ambayo ndani yake alitamani kuona maelewano, mapatano, mshikamano na alitamani kufanya siasa za kidugu.
“Ndoto hizo leo tumshukuru Mwenyezi Mungu kwani Rais Samia Suluhu Hassan anaziishi na anaziendeleza, tumwombee kwa Mwenyezi Mungu Rais Samia aweze kuendana vyema na maoni na dira ya watangulizi waliotangulia katika nchi yetu. Kwa hiyo wakati tunamwombea Dk. Omari Ali Juma, tumwombee na Rais Samia Suluhu Hassan aweze kutenda mema yale ambayo waliotangulia waliyafanya,” alisema.
KABURINI KWA MAALIM SEIF
Akiwa katika kaburi la Maalim Seif, Shaka alisema yeye na msafara wake wamefika katika kaburi hilo kwa ajili ya kumuombea Dua Maalim Seif ambaye Mwenyezi Mungu amemuita na ameitikia.
“Wakati tunafanya hivi tunakumbuka ama tupo kwenye kumbukizi ya miaka 30 ya mfumo wa vyama vya siasa. Wakati tunakumbuka Maalim Seif Sharif Hamad tunakumbuka macho wake alioutoa katika nchi hii kuhuisha na kustawisha siasa za Tanzania.
“Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na kufanya siasa, alitanguliza huruma, alitanguliza upendo, lakini alikuwa na uvumilivu uliopitiliza katika kuendesha siasa za nchi hii, nyakati zote hata pale Chama Cha Mapinduzi kilipofungua milango ya maridhiano na mazungumzo Maalim Seif alitanguliza maslahi mapana ya Watanzania, lakini alitanguliza malahi mapana zaidi ya wazanzibari pamoja na kuwaunganisha,” alisema.
Akifafanua kuwa, hilo ni funzo kubwa kwa kizazi kilichobaki ambapo alitaka kuishi kwa kufuata nyayo zake badala ya kuongozwa katika jazba, chuki na mpasuko ndani ya Jamii na nchi kwa ujumla.
Alisema ni vyema Watanzania wakarudi kufuata nyayo za waliotangulia katika miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, hivyo alisisitiza kuwa bado kuna nafasi ya kujenga leo ya Taifa na bado kuna nafasi ya kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya vizazi vijavyo.
“Maalim Seif amefariki lakini ametuachia funzo kubwa, ametuachia deni kubwa ambalo limetuletea amani, umoja na mshikamano, ninachoweza kusema ni kwamba bila busara na hekima ya viongozi waliotangulia, matunda haya tuyaonayo leo yasingalikuwepo, Dunia leo hii imepata funzo kubwa kutoka Zanzibar na Tanzania, ndiomana leo hii tumefika hapa Mtambwe kukiwa na amani, wamoja bila kujali itikazi zetu za siasa, wala dini.
“Tumesimama wamoja na kumuenzi Maalim Seif Sharif Hamad hizi ni mbegu njema ambazo alizipanda kwa wazanzibari, alizipanda kwa Watanzania
Katika hatua nyingine, familia za viongozi hao kupitia wawakikishi wakiizungumza katika ziara hiyo ya shaka, waliiomba serikali kuboresha barabara zinazokwenda katika makaburi hayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema wamekuwa wakipokea ugeni wa viongozi mbalimbali wanaifika kuzuru makaburi hayo lakini miundombinu ya barabara sio rafiki, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa.