Silvia Mchuruza,Bukoba, Kagera
Katika harambee iliyofanywa na kanisa Katoliki kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Rulongo, kijiji cha Rwagati, kata ya Kashasha Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amewasihi wananchi wa Wilaya ya Muleba kuendelea kuienzi na kuitunza amani kwa maendeleo ya Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa harambee hiyo, Mhe. Nguvila amewaeleza wananchi kuwa viongozi wa Dini, viongozi wa Serikali na viongozi wa Kimila wanao wajibu wa kuhakikisha wanashirikiana kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
“Yapo matukio ya kujinyonga na ukatili wa kupiga mtu mpaka kuua, sisi kama viongozi haya mambo ni lazima tuyakemee na sisi kama waumini ni lazima tukemee hizi roho ambazo zinakwenda kinyume na mapenzi ya Mungu” amesema Mhe. Nguvila.
Aidha, amewasihi pia wananchi kuhakikisha wanaachana na tabia ya uuzaji wa kahawa kwa njia ya magendo na kuwasihi kuuza kahawa kwa njia ya mnada ambao itawasaidia wakulima wa zao la kahawa kunufaika na zao hilo.
Sambamba na hayo amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katiza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 23, Agosti 2022 zoezi ambalo lengo lake ni kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Mhe. Costansia Buhiye ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi katika Harambee hiyo, amewasihi wananchi kuhakikisha wanaimarisha upendo na ushirikiano ili nchi iweze kuwa na amani.
Ujenzi wa Kanisa hilo ulianza rasmi tarehe 8/6/ 2022 ambapo mpaka sasa upo hatua ya msingi ambao umegharimu kiasi cha Tsh. Milioni 6.7 na mpaka kukamilika kwa jengo la kanisa hilo inakadiriwa kugharimu kiasi cha Tsh. Milioni 122.