Mwanaharakati anayetetea watoto wa kike katika shule za msingi wenye mahitaji maalumu, Janeth John (aliyekaa mstari wa mbele wa kwanza kushoto) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa 3 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA), akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Furaha iliyopo Mjini Tabora ya watoto wenye mahitaji maalumu baada ya kuwatembelea hivi karibuni na kuwapa semina.
……………………………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
WANAFUNZI wa kike wenye ulemavu wa aina mbalimbali wanaosoma katika shule za msingi Mkoani Tabora wameaswa kujitambua ili kuweza kukabiliana na changamoto wanazopitia katika makuzi yao
Ushauri huo umetolewa juzi na Mwanaharakati wa kutetea na kupigania haki za wanawake, watoto pamoja na watu wenye ulemavu, Janeth John ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa 3 katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA) alipokuwa akiongea na gazeti hili.
Janeth ambaye ni mwanafunzi mwenye usikivu hafifu, mwandishi wa vitabu na mshauri wa masuala ya kijamii alisema mtoto wa kike akijitambua anaweza kufanya mambo makubwa yatakayomwezesha kutimiza ndoto zake kimaisha.
Alibainisha kuwa programu ya ‘Sema Usikike’ambayo amekuwa akiitoa kwa watoto wa kike wa kuanzia darasa la 5 hadi 7 katika shule mbalimbali imelenga kuwaongezea uelewa, kutambua wajibu wao na kuongeza bidii katika masomo.
Alifafanua kuwa hivi karibuni walitembelea shule ya msingi Tabora -Viziwi na kukutana na wanafunzi wa kike wa darasa la 5-7 wenye mahitaji maalumu na kuwapa elimu ya umuhimu wa kujitambua na kujua wajibu wao katika jamii.
Janeth aliongeza kuwa mtoto wa kike au wa kiume mwenye mahitaji maalumu anapaswa kuelewa kuwa ulemavu sio ugonjwa, na kwamba hakuna mwanadamu aliyekamilika, kila mmoja ana ulemavu wake, hivyo anapaswa kuweka juhudi kubwa katika kile anachofanya na sio kujichukulia kwamba hawezi.
‘Elimu hii ni muhimu sana kwa watoto wa kike wa shule za msingi kwani itawajengea msingi wa kujiamini, wakijitambua watasoma kwa bidii, hawatakubali kunyanyapaliwa, kudharauliwa au kukatishwa tamaa na mtu yeyote ikiwemo kudanganywa na vijana wa kiume’, alisema.
Alibainisha kuwa dhamira yake ni kuhakikisha programu hii inawafikia wasichana wa darasa 5 hadi 7 katika shule zote zenye watoto wenye mahitaji maalumu nchini na hasa wale walioko vijijini.
Janeth aliongeza kuwa maono yake ni kuanzisha taasisi ya kutetea, kupigania na kuelimisha mtoto wa kike hususani mwenye mahitaji maalumu ili ajitambue na kusimamia haki yake, lengo likiwa kuwafikia wasichana wengi zaidi
Alibainisha lengo la programu hiyo kuwa ni kutoa mafunzo ya elimu ya kijinsia kwa wasichana wa darasa la 5, 6 na 7 wa shule za msingi ili waweze kujitambua na kukabiliana vizuri na changamoto za ukuaji wao ikiwemo kutambua uwezo wao ili watimize ndoto zao.
Aliomba serikali, mashirika, watu binafsi, makampuni na wadau mbalimbali kumuunga mkono kwa kufadhili programu hiyo ili aweze kuwafikia mabinti wengi zaidi nchini.