Na Damian Kunambi, Njombe
Naibu waziri wa maji Maryprisca Mahundi amewataka vijana kujihusisha na michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu ili kuweza kujipatia kipato na kuboresha afya zao.
Hayo ameyasema wilayani Ludewa mkoani Njombe alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mashindano ya mpira wa miguu msimu wa tatu yajulikanoyo kama Kuambiana Cup ambayo huandaliwa na Imani Haule yakihusisha kata 5 za tarafa ya masasi chini ya udhamini wa Kuambiana Investment yakiambatana na kauli mbiu isemayo “MTU KWAO REJESHA FURAHA NYUMBANI”.
Aidha kwa upande wa mwandaaji wa mashindano hayo Imani Haule (Kuambiana) ambaye pia ni mkurugenzi wa Kuambiana Investment amesema mashindano haya yamekuwa na matokeo mazuri kwa washiriki huku akiwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono wachezaji hao katika suala zima la usafiri ili vijana hao waweze kutimiza ndoto zao.
“Vijana wengi wanahitaji kushiriki michezo hii lakini changamoto iliyopo ni usafiri wa kutoka vijijini kwao na kuwafikisha katika eneo la mashindano hivyo nawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kuwaunga mkono Vijana hawa ili waweze kusafirishwa”, Amesema Haule.
Ameongeza kuwa yeye ni mwana soka na mzaliwa wa wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe hivyo amekuwa akitamani kuona vijana kutoka maeneo ya mkoa huo na hasa Ludewa wakipata nafasi za kuchezea timu kubwa hapa nchini.
Sunday Deogratius ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa, amempongeza kuambiana kwa kukumbuka vijana wa nyumbani kwao kwakuwa watu wengi wamekuwa wakisahau kuinua wengine waliobaki nyuma.
“Nikupongeze sana kwa moyo uliouonyesha kwa kuwakumbuka vijana katika vipaji vyao, huu ni mfano mzuri ambao unapaswa kuigwa na kila mtu, na sisi kama serikali tutahakikisha tunakuunga mkono katika hili”, Amesema Deogratius.
Mashindano hayo yanafanyika ikiwa ni msimu wa tatu toka kuanzishwa kwake mwaka 2020 na katikati mashindano ya hivi sasa yamezinduliwa na timu ya Masasi ya wilaya ya Ludewa pamoja na timu ya polisi ya wilaya ya Nyasa ambapo Masasi walifunga magoli matatu kwa moja na kujipatia fedha kiasi cha sh. 300,000, kombe pamoja na Medani huku timu ya polisi ikiondoka na medani na sh. 200,000.