Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack wakitazama Filamu ya The Royal Tour kwenye uwanja wa Wandorwa, Ruangwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipowaongoza wananchi wa wilaya ya Ruangwa kutazama Filamu ya The Royal Tour kwenye uwanja wa Wandorwa.
Wananchi wa Ruangwa wakitazama Filamu ya The Royal Tour kwenye uwanja wa Wandorwa, Julai 8, 2022. Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa ni Waziri Mkuu na Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………..
*Aagiza kuibuliwa kwa fursa za utalii ili kunufaika na watalii wanaoingia nchini
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri za Wilaya nchini kuweka mipango ya kuibua fursa za utalii ili ziweze kunufaika na idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini baada ya hamasa kubwa iliyochechewa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya The Royal Tour.
Mheshimiwa Majaliwa alitoa agizo hilo jana usiku (Ijumaa, Julai 08, 2022) alipouongoza umati mkubwa wa wananchi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kutazama filamu ya The Royal Tour kwenye uwanja wa Wandorwa wilayani hapa.
Waziri Mkuu alisema filamu ya The Royal Tour ina nafasi ya kuimarisha shughuli za maendeleo katika mikoa yote nchini ukiwemo na mkoa wa Lindi ambao una vivutio vingi vya uwekezaji na utalii, hivyo kila wilaya itumie fursa hiyo kuainisha vivutio vilivyopo na kuvitangaza mfano viboko vyenye ualbino ambavyo vinapatikana wilayani Kilwa.
“Viboko hawa ni wa kipekee sana hawapatikani sehemu yoyote na ni kivutio kizuri cha utalii kwani unaweza kuwaita na wakaibuka juu na ukiwaambia wazame wanazama, hivyo Maafisa Utalii mlioko makao makuu ya wilaya ya Kilwa wekeni mpango mzuri wa kutangaza viboko hawa, ni kivutio kikubwa cha utalii”
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema Rais Mheshimiwa Samia moja ya mkakati wake ni kuboresha na kukuza uchumi na amewahakikishia Watanzania na ulimwengu kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuja kuwekeza na ametoa fursa za uwekezaji nchini.
Alisema katika ziara zake anazozifanya nje ya nchi moja kati ya ajenda yake ni kuwakaribisha wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, madini, biashara, utamaduni na sanaa.
Mheshimiwa Majaliwa alisema Rais Mheshimiwa Samia amekuja na ubunifu wa kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo nchini kwa kupitia filamu ya The Royal Tour, hivyo aliwasisitiza Watanzania wakiwemo wananchi wa wilaya ya Ruangwa kuitumia fursa hiyo kwa kuibua miradi ya uwekezaji itakayowainua kiuchumi na kutengeza ajira hususan kwa vijana.
“Migodi mikubwa ya madini mbalimbali yakiwemo ya Bunyu (Graphite) inayotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni katika wilaya yetu ni fursa ambayo wana-Ruangwa tunapaswa kuichangamkia kwa kuwekeza kwenye miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali itakayowawezesha wageni kupata huduma muhimu za kijamii kama malazi, chakula na usafiri.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack alisema mkoa huo tayari umeanza kunufaika tangu filamu hiyo izunduliwe, ambapo idadi ya watalii imeongezeka pamoja na wafanyabiashara wanaoingia kwa ajili ya kutafuta maeneo ya uwekezaji.”Fursa za utalii na uwekezaji mkoani Lindi ni nyingi sana wananchi wanatakiwa kuzichangamkia.”
Filamu ya kihistoria ya Royal Tour ilizinduliwa nchini tarehe 28 Aprili, 2022 Jijini Arusha, filamu hiyo, imechangia kuimarisha shughuli za utalii na kusaidia kutangaza urithi wa utalii uliopo Tanzania.