Na.Farida Saidy,Morogoro
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajia kuanza rasmi ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Morogoro siku ya Jumamosi tarehe 14 Septemba mwaka huu ambapo atakagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya tano Mkoani humo.
Akitoa taarifa ya Ujio wa Mhe. Majaliwa kwa waandishi wa habari Ofisini kwake Septemba 13 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amesema Waziri Mkuu anatarajia kukamilisha ziara hiyo Septemba 18 mwaka huu baada ya kutembelea Halmashauri sita kati ya tisa za Mkoa huo.
Dkt. Kebwe amesema, Halmashauri atakazotembelea Mhe. Waziri Mkuu ni pamoja na Halmashauri za Wilaya za Kilombero, Malinyi, Ulanga, Ifakara Mji, Kilosa na Morogoro DC ambapo ataweka mawe ya msingi na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano pamoja na kuongea na wananchi wa maeneo ambayo yameandaliwa.
Amesema katika ziara hiyo Mhe. Majaliwa atakagua miradi mbalimbali pamoja na kuongea na wananchi katika baadhi ya maeneo atakayotembelea hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo wa Kitaifa.
“Wakazi wote ambao wapo katika viunga vya mkoa wa Morogoro na katika maeneo ambayo Mhe. Waziri Mkuu atatembelea miradi au kuongea na wananchi basi mjitokeze kwa wingi kumpokea kiongozi wetu”, Alisema Dkt. Kebwe.
Aidha Dkt. Kebwe amewataka wakuu wote wa Wilaya ambazo Mhe. Waziri mkuu atatembelea wahakikishe wanasimamia vizuri maandalizi ya ujio wa Kiongozi huyo ili kuepuka kukwamisha Ratiba ya Ziara hiyo.
Amesema katika siku ya kwanza ya ziara yake Mhe. Majaliwa anatarajia kupokelewa Ifakara iliyopo Wilayani Kilombero hivyo amewaagiza viongozi wa Wilaya zilizopo jirani na eneo hilo kushiriki katika shughuri ya kumpokea kiongozi huyo.
Akiwa Wilayani Kilombero, Mhe. Waziri Mkuu atatembelea vituo vya Afya Mchombe na Kibaoni pamoja na kutembelea Kiwanda cha Sukari cha Kilombero.
Aidha Mhe. Waziri Mkuu atatembelea Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ambapo ataweka jiwe la msingi Jengo la Ofisi ya Halmashauri hiyo na kufanya Mkutano wa Hadhara na wananchi wa malinyi mjini.
Waziri Mkuu ataelekea Mahenge Wilayani Ulanga ambapo atapata fursa ya kutembelea Hospitali ya Wilaya hiyo na kisha kuwasalimia Wananchi wa Mahenge. Mhe. Waziri Mkuu ataendelea na ziara yake kwa kutembelea kituo cha Afya kibaoni, kuwasalimia wananchi wa eneo la Ifakara kisha ataelekea Kidatu kutembelea Kiwanda cha Sukari cha Kilombero.
Waziri Mkuu anatarajia kutembelea kituo cha Afya cha Malolo kilichopo katika Wilaya ya Kilosa ambao pia atapata fursa ya kuwasalimia wananchi wa Malolo na Mikumi.
Mhe. Waziri Mkuu atahitimisha ziara yake kwa kutembela makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro pamoja na kuweka Jiwe la Msingi Hospitali ya Wilaya hiyo ambapo pia atawasilimia wananchi na watumishi wa Halmashauri hiyo kabla ya kuelekea jijini Dar es Salaam.