Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya bajeti ,Daniel Sillo akizungumza na waandishi wa habari katika ziara hiyo jijini Arusha
Jengo la mradi huo katika chuo cha ufundi Arusha .
Kamati ya Bunge ya bajeti ikisikiliza maelezo ya mradi katika chuo cha ufundi Arusha( ATC).
……………………………………………..
Julieth Laizer, Arusha
Arusha.Kamati ya Bunge ya bajeti imefanya ziara katika chuo cha ufundi Arusha(ATC) katika kutembelea na kufuatilia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa, maabara na ofisi za chuo hicho.
Akizungumza katika ziara hiyo Naibu waziri wa elimu sayansi na teknolojia , Omary Kipanga amesema mradi huo unatekelezwa na fedha za Uviko 19 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan umetoa fursa ya kuimarisha stadi za ujuzi kwa wanafunzi wa ufundi walioshiriki mafunzo kwa vitendo katika mradi.
Aidha ameishukuru serikali kwa kuboresha vyuo mbalimbali ikiwemo kujenga vyuo vinne vya ufundi katika maeneo ambayo hayakuwa na vyuo hivyo ambapo shs 20 bilioni zimepelekwa kwa ajili ya kujenga vyuo vinne katika mikoa ya Rukwa,Njombe na Simiyu.
Naye Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Dk Mussa Chacha amesema chuo hicho kinaongoza kwa kutoa mafunzo tafiti na ushauri wa kitaaluma kwa kuangalia mahitaji ya soko huku washirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha taaluma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti ,Daniel Sillo amesema kamati hiyo ndio yenye jukumu la kupitisha matumizi ya fedha zilizopatikana na kutembelea miradi hiyo ili kupata fursa za kuishauri serikali kwa jinsi wanavyotekeleza miradi hiyo huku akitoa wito kwa wakufunzi na walimu wa chuo hicho kulinda na kutunza majengo hayo kwa sasa na vizazi vijavyo.
Sillo amesema kuwa ,baada ya kukagua ujenzi wa jengo hilo linalogharimu kiasi cha sh,bilioni 2.27 ambapo hatua iliyofikiwa kwa sasa ni asilimia 90 wameridhishwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Amesema fedha hizo zimesaidia ujenzi wa madarasa nane yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 880 kwa wakati mmoja,maabara sita zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 270 kwa wakati mmoja ikiwemo ofisi 26 zenye uwezo wa kuchukua watumishi 104.
“Hapa tumeona jinsi fedha za Uviko-19 zinavyofanya kazi,tunampongeza Rais Samia kwa kuhakikisha vyuo vya ufundi vinajengwa ili kusaidia jamii kuongeza ujuzi na kuleta tija hapo baadae “amesema.
Hata hivyo Mhandisi wa mradi huo na Meneja wa kitengo cha uzalishaji na usimamizi wa miradi chuo cha ufundi Arusha, Faraji Magania ameeleza kuwa jengo hilo lipo katika hatua ya umaliziaji na linatarijia kukamilika kwa wakati kabla ya mwaka na masomo 2022/2023.