Na John Walter-Manyara
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba, amewataka watumishi idara za maji nchini kufanya kazi kwa kasi kufikia malengo ya serikali ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama.
Ametoa wito huo leo julai 6,2022 wakati akifungua Kikao kazi cha wakuu wa idara ya biashara wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Good life Hotel mjini Babati.
Amesema Upatikanaji wa maji ni nyenzo muhimu katika kupunguza ukali wa maisha ikiwemo magonjwa na kuokoa dola nne za matibabu ambayo itaelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.
Aidha amesema wizara hiyo haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwaondoa katika nafasi za kazi zao mameneja wa biashara katika mamlaka za maji ambao wanashindwa kuzisaidia mamlaka hizo kujiongezea mapato na kufikia lengo la kuondokana na utegemezi na kushindwa kulipa baadhi ya huduma ikiwemo nishati ya umeme.
Pamoja na mambo mengine Mhandishi Nadhifa amezitaka mamlaka hizo za maji nchini Kukusanya madeni kitaalamu bila kugombana na wateja ili kuzidi kujenga mahusiano mazuri.
Kikao hicho cha siku mbili kimelenga kubadilishana uzoefu katika kutoa huduma za maji kwa wateja na namna ya kufikia malengo katika ukusanyaji wa mapato kwenye mamlaka hizo.
Mwenyekiti wa Mameneja Biashara Mamlaka za maji Biswalo Bernard ameeleza kwamba mamlaka hizo huwenda zikafikia lengo la ukusanyaji wa mapato na kuondokana na upotevu wa maji pamoja na uchelewashwaji wa malipo kutoka kwa wateja wa maji endapo serikali itaruhusu matumizi ya mita za maji za malipo kabla.