Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu toka kushoto) akiwa na wataalamu mbalimbali wakati wa ukaguzi wa barabara zilizopo chini ya usimamizi wa Wakala wa barabara za Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA) katika mji wa Namanyere katika Wilaya ya Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka Kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (kushoto) Mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Boniface William ( wa pili toka kulia) pamoja na Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya (kulia) wakitembea wakati wa ukaguzi wa barabara zilizopo chini ya usimamizi wa Wakala wa barabara za Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA) katika mji wa Sumbawanga, Wilayani Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo pamoja na Wataalamu wengine wakikagua mitaro katika moja ya barabara za mji wa Sumbawanga.
…………………
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha anatekeleza ahadi zake alizoahidi kipindi cha kampeni baada ya kutembelea barabara zinzoendelea kujengwa katika mji mdogo wa Namanyere, Wilayani Nkasi na kuona kasi ya ujenzi wa barabara hizo ikiendelea vizuri.
Amesema kuwa ahadi ya mheshimiwa rais ni kujenga barabara zenye jumla ya kilometa tano katika mji na mpaka kufikia mwezi Disemba mwaka 2019 zitakuwa zimefikia jumla ya kilometa 3.95 ambayo ni sawa na asilimia 79 ya utekelezaji wa ahadi zake na hivyo kumtaka mkandarasi nayeendelea na ujenzi wa barabara ya kilometa moja afanye haraka kumalizia ujenzi huo ili wananchi waweze kutumia barabara ambazo zimefungwa kwa muda wa mwaka ili kupisha ujenzi.
“Huyu mkandarasi anayejenga kilometa moja kwa kiwango cha lami kazi yake inasuasua kwasababu mradi huu ulipaswa kukamilika mwezi wa sita mwaka huu na sasa ni mwezi wa tisa, kazi haijakamilika lakini pia kuna kero ambazo zipo ndani ya barabara hizi, kuna vivuko vimewekwa vya muda na kwengine hakuna, watu wanapata shida kuvuka mitaro kwenda kufanya biashara zao lakini pia kwenye matolea ya barabara kuna vifusi, hivyo nakupa siku 12 utoe vifusi na ujenge vivuko kwenye mitaro,” Alisisitiza.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo ili kutimiza ahadi za Mheshimiwa Rais Mratibu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji Tanzania (TARURA) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Boniface William alisema kuwa mbali na kujitahidi kuhakikisha barabara hizo zinajengwa kwa wakati lakini kumekuwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti pamoja na upatikanaji wa malighafi za ujenzi wa barabara hizo hasa kokoto.
“katika utekelezaji wa hii miradi kumekuwa na changamoto mbalimbali, changamoto mojawapo ni ufinyu wa bajeti, fedha tunayotengewa kulingana na hali halisi ya ‘site’ unakuta ile fedha ni kidogo kiasi kwamba kama ile barabara ya salala ilikuwa tutengeneze kilometa moja lakini kwa milioni 350 tulishindwa kutengeneza kilometa moja kwahiyo tukaweza kutengeneza mita 700 pekee, tatizo jingine ni malighafi kwa maana ya kuwa na chanzo kimoja cha kokoto katika mkoa, hii inachelewesha kazi,” Alisema.
Katika hatua nyingine, Mh. Wangabo wakati alipomaliza kutrembelea barabara zenye jumla ya kilometa moja katika manispaa ya Sumbawanga amewataka wakandarasi wazawa wanaopewa kazi za ujenzi na TARURA kuhakikisha wanaheshimu na kuzingatia masharti ya mikataba ili kufanya kazi kwa wakati na kuongeza kuwa ikiwa wakandarasi hao hawataonyesha uaminifu katika kazi hizo ndogo itakuwa vigumu kwao kupewa miradi mingine mikubwa.
Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Nkasi wametengewa bajeti ya shilingi milioni 500 wakati TARURA upande wa Manispaa ya Sumbawanga wametengewa bajeti ya shilingi milioni 460 ili kuendelea kukamilisha ujenzi wa barabara katika kutimiza ahadi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli.