********************
Serikali imesema itaendelea kushughulikia na kutafuta ufumbuzi kwa changamoto mbalimbali zitakazojitokeza baada ya kuanza kutumika kwa mfumo wa tiketi za mabasi za kielektroniki nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire, amesema pamoja na utatuzi wa changamoto zitakazojitokeza kupitia tiketi hizo matumizi ya mfumo huo utampunguzia abiria adha ya kupita kwa mawakala na hivyo kuwa na uhakika na safari yake bila kulanguliwa tiketi.
Katibu Mkuu Migire amewapongeza Chama Cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), na Wadau wengine wa usafirishaji kwa kutoa ushirikiano kwa kipindi cha miezi mitatu ya majaribio ya mfumo huo na kusema kuwa zoezi hilo likitekelezwa kwa uaminifu litarahisisha shughuli za usafiri kwa wamiliki na abiria kwa ujumla.
“Nichukue fursa hii kuwaomba TABOA na wadau tuendeleze ushirikiano katika utekelezaji wa mfumo huu wa tiketi kwani manufaa yake yataonekana muda mfupi ujao kwa wamiliki na abiria”, amesema Katibu Mkuu Migire.
Katibu Mkuu Migire ameeleza kuwa utekelezaaji wa zoezi hilo ni matokeo ya vikao vya mara kwa mara ambavyo Sekta imekuwa ikivifanya na kuwahusisha wadau wote wa usafirishaji lengo likiwa ni kuboresha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kwa upande wake, Katibu wa TABOA, Priscus Joseph, amesema tangu tarehe mosi Julai ambayo mfumo huo umeanza kutumika abiria yoyote anayekata tiketi anaweza kukata popote na kupata tiketi hiyo kwa urahisi.
Naye, Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Kampuni ya mabasi ya Super Feo na Selou Express, Francis Sengo, amesema kuwa toka aanze kutumia mfumo huu umemsaidia na umerahisisha katika usimamizi wa mapato na ukataji tiketi kwani abiria anakata tiketi kwa mtandao hivyo anajua idadi ya abiria wanaosafiri kila siku tofauti na zamani kabla ya mfumo haujaanza.
Mfumo wa tiketi za kielektroniki umeanza kutumika rasmi tarehe 1 Julai kwa mabasi yote nchini na kupitia mfumo huo abiria ataweza kukata tiketi na kuilipia tiketi moja kwa moja kwa njia ya mtandao bila kupitia kwa mawakala wa mabasi.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliiano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)