ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Tanzania Church of God International (T.C.G.I) katika Manispaa ya Kahama, Askofu Saimon Nkwabi amesema viongozi wa dini nchini wataendelea kuliombea Taifa lidumu katika amani na kupata maendeleo .
Pia watamwombea Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuliongoza taifa letu kwa amani, upendo na usawa na kuwataka wananchi kumuunga mkono kwa kazi anayoifanya ya kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali na maridhiano kama taifa .
Baba Askofu Nkwabi alisema hayo leo asubuhi alipomtembelea Khamis Mgeja ofisini kwakwe Kahama motel na kufanya mazungumzo na kubadilishana mawazo kuhusu mustakabali wa nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Alisema viongozi wa dini kwa pamoja wataendelea kumwombea Rais Samia aliongoze taifa kwa weledi,haki,usawa, upendo na amani ili kuhakikisha watanzania wanapata maendeleo ya kiuchumi,kisasa na kijamii.
Askofu Nkwabi alisema Rais Samia ameonyesha uwezo mkubwa katika uongozi wake kwa vitendo, ana maono ya kulifanya taifa kuwa na nguvu kiuchumi na ana anahangaika kutafuta na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
“Ni kiongozi jasiri mwenye maono, mnyenyekevu na asiyejikweza licha ya kuwa ni mwanamke.Tunapaswa kumwombea na kuunga mkono jitihada zake za kuiletea nchi maendeleo ya kisekta,”alisema kiongozi huyo wa kiroho.
Pia Askofu Nkwabi alimuombea na kumtakia kheri Mgeja katika maisha yake ya kila siku na kumuomba Mungu amzidishie hekima na busara, amkinge na shari zozote .
Aidha alimpongeza Mgeja kwa kuwa mpenda haki,mkweli mwenye kushirikiana vizuri na jamii bila ubaguzi wa dini, ukabila na ukanda na kuwaomba wanasiasa wengine kuiga mfano huo.
Alisema viongozi hao wa dini wana mchango kubwa kwa nchi na jamii, wameendelea kuliombea taifa letu na viongozi wetu akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan,Makamu wa Rais, Dk.Isdory Mpango, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Dr. Hussein Mwinyi akiwemo Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa na wengine.
“Baba Askofu Nkwabi tunawashukuru kwa kuendeleza na kudumisha amani ya nchi yetu na hatimaye kujiletea maendeleo kwa mchango wenu wa maombi na ujenzi wa jamii kiroho,”alisema Mgeja.ssss