Na Marco Maduhu, SHINYANGA
KAMISAA wa zoezi la kuhesabiwa Sensa ya Watu na Makazi hapa Nchini Anne Makinda, amelipongeza kundi la Whatsapp la SHYTOWN VIP la Mjini Shinyanga, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambalo litafanyika Agosti 23 mwaka huu, huku Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akiahidi kuvunja Rekodi kwa nchi nzima kulifanya zoezi hilo kikamilifu kwa kuandikisha idadi ya watu wengi.
Makinda ametoa pongezi hizo Jana Julai 2, 2022, wakati akishiriki hafla ya kuhamasisha Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, washiriki kwa wingi katika zoezi hilo la kuhesabiwa Sensa ya watu na makazi, hafla iliyoandaliwa na kundi la Whatsaap SHYTOWN VIP na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama.
Akizungumza kwenye hafla hiyo amesema kikundi hicho cha Group la Whatsapp SHYTOWN VIP, wamefanya jambo kubwa sana la kushirikiana na Serikali kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo la kuhesabiwa Sensa, ambalo litaisaidia kupata idadi ya watu wake kamili na kupanga mipango ya kuwatekelezea miradi ya maendeleo kulingana idadi yao.
“Nashukuru sana kwa makaribisho ya kushiriki na ninyi katika jambo hili la muhimu sana la kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la kuhesabiwa Sensa, hakika wana SHYTOWN VIP Mme muheshimisha sana Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, mimi nilikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma lakini siku bahatika kuwa na kitu kama hiki, hili ni jeshi kubwa sana la mama,”amesema Makinda.
Katika hatua nyingine Makinda ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, amewasihi Watanzania siku hiyo ya zoezi la kuhesabiwa Sensa ya watu na Makazi, wajitokeze kwa wingi kuhesabiwa pamoja na kukumbusha wao kwa wao ili Serikali itimize malengo yake ya kuwa na idadi kamili ya watu wake.
Amesema siku ya zoezi hilo wananchi wanapaswa kutoa taarifa za ukweli na sahihi kwa Makarani na wasifiche taarifa zao na kusema uongo ili kuto haribu zoezi hilo na iwe virahisi kwa Serikali inapokuwa ikipanga mipango yake ya maendeleo kwa wananchi wa eneo fulani iwe na idadi yao kamili na kuwatimizia mahitaji yao wote.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amesema wamejipanga vyema kuhamasisha wananchi wa Mkoa huo kushiriki kwa wingi kuhesabiwa, na wanataka kuvunja Rekodi nchi nzima ili wawe wakwanza kulifanya zoezi hilo kikamilifu.
“Naomba nikuahidi Kamisaa wa Sensa, kwa vibe !ambalo umeliona kwa vijana hawa (SHYTOWN VIP),wamejipanga kupiga debe hili la kuhamasisha wananchi kushiriki kuhesabiwa Sensa hadi Agost 23 mpaka wananchi waelewe Sensa ni nini na wajitokeze kuhesabiwa, na sisi Shinyanga tunataka tuwe wa kwanza tuvunje Rekodi kuhamasisha watu wanajitokea kwa wingi na kuhesabiwa hiyo ni ahadi yetu,”amesema Mjema.
Kwa upande wake Mtakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Makao Makuu Dodoma Pastory Ulimali, amesema zoezi la Kuhesabiwa Sensa ya watu na Makazi mwaka huu (2022) ni la sita hapa nchini, na wanatarajia kuandikisha watu Milioni 64.
Amesema zoezi la kuhesabiwa Sensa hapa nchini lilianza mwaka 1967 na waliandikishwa watu Milioni 12.3, mwaka 1978 watu Milioni 17.5 Mwaka 1988 watu Milioni 23.1, Mwaka 2002 watu Milioni 34.4, na Mwaka 2012 watu Milioni 44.9 na zoezi hilo la kuhesabiwa Sensa hufanyika kila baada ya miaka 10.
Mwenyekiti wa kikundi hicho cha Whatsap Shytown VIP Mussa Ngangala, amesema wapo wanachama 411 na kila mwaka wamekuwa na utaratibu kukutana na kufanya shughuli za kijamii, na mwaka huu wameangukia kwenye zoezi la Sensa na kuamua kuungana na Serikali kuhamasisha wananchi washiriki kwa wingi kuhesabiwa.