Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi wa Operesheni wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC) Bw. Andreas Anderson (Katikati) alipowasili katika chuo hicho kwa ajili ya ufunguzi wa Tamasha la Kiswahili leo Jijini Arusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiingia katika ukumbi wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa ( MS TCDC) ufunguzi wa Tamasha la Kiswahili leo Jijini Arusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na wadau na wataalamu wa kiswhali katika ukumbi wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa ( MS TCDC) wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Kiswahili leo Jijini Arusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akisoma maandishi yaliyoandikwa katika mkeka ikiwa ndiyo kiashiria cha kufungua Tamasha la Kiswahili leo Jijini Arusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akionyesha ujumbe wa maandishi uliwahi kusema na Baba wa taifa Hayati Julius Nyerere (Taifa lolote lisilokuwa na Utamaduni wake ni Taifa Mfu) wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Kiswahili leo Jijini Arusha.
Kikundi cha Ngoma kikitoa burudani kwa washiriki wa Tamasha la Kiswahili (hawapo katika picha) wakati wa ufunguzi wa Tamasha hilo leo Jijini Arusha.
(Picha na Lorietha Laurence-WHUSM,Arusha).
………………..
Na Lorietha Laurence- WHUSM,Arusha
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe awapa kongole wadau na wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini na nchi za jirani (Jumuiya ya Afrika ya Mashariki) waliojitokeza kwa wingi kushiriki ufunguzi wa Tamasha la Kiswahili Jijini Arusha.
Dkt. Mwakyembe ametoa pongezi hizo leo Jijini hapo wakati wa ufunguzi wa tamasha hilo lililokuwa na kauli mbiu ya “Tukienzi Kiswahili na Utamaduni kama nyenzo muhimu za maendeleo” lengo ikiwa ni kuibidhaisha lugha hiyo katika sehemu mbalimbali duniani.
“jukwaa hili ni fursa nzuri ya kuhakikisha tunatoka na nia moja ya kuweza kuifikisha lugha yetu ya Kiswahili katika maeneo mbalimbali duniani ili ifahamike na kutumika kama lugha ya mawasiliano” Dkt. Mwakyembe.
Aidha aliongeza kwa kusema kuwa tayari lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa kwa upande wa Afrika ambapo Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika imeipitisha lugha hiyo kuwa miongoni mwa lugha nne rasmi za mawasiliano kwa mwanachama hao.
“Hapa juzi katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini Mwa Afrika uliofanyika tarehe 18 Agosti 2019 tumeshuhudia Kiswahili kimekubaliwa kuwa moja ya lugha nne rasmi ya mawasiliano kwa jumuiya hiyo”
Anazidi kueleza kuwa azma ya Rais wa awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha lugha ya Kiswahili inabidhaishwa na kufanywa kuwa chanzo muhimu cha ajira na mapato kwa wataalamu wa lugha hiyo nchini na nje ya nchi.
Naye Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Dkt. Selemani Sewange ameeleza kuwa tamasha hilo ni la kipekee kuandaliwa na Baraza lake ambapo mada mbalimbali zitakazowasilishwa zenye lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu lugha ya Kiswahili.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo Cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa ( MS TCDC ) Dkt. Servacius Likwelile aliwashukuru wadau , wataalamu na wote waliojitokeza kufanikisha tamasha hilo .
Tamasha hilo limefanyika kwa mara ya kwanza baada ya kusimama kwa muda wa miaka 12 , ambapo mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2007 kwa jina ya Siku ya Kiswahili .