Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Thomas Rutachunzibwa akizungumza wakati wa kufungua maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya yaliyoandaliwa na OJADACT
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wa kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifuTanzania (OJADACT) Edwin Soko akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya
Waandishi wa habari wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Thomas Rutachunzibwa baada ya kufungua maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya yaliyofanyika leo hii Jijini Mwanza
************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Waandishi wa habari Mkoani Mwanza wametakiwa kutumia taaluma yao vizuri katika kuielimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 30,2022 na mwenyekiti wa chama cha kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu Tanzania (OJADACT) Edwin Soko, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya yaliyoandaliwa na chama hicho.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo “Tujadiliane kwa pamoja ili tuweze kukomesha matumizi ya dawa za kulevya”yamefanyika Jijini Mwanza kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Amesema watumiaji wa dawa za kulevya wanapata athari kubwa ikiwemo ya kuporomoka kiuchumi,kushindwa kuendesha familia,kuongea mwenyewe na muda mwingine kutumia nguzu katika kukaba watu ili wapate hela ya kununua dawa hizo,hivyo waandishi wa habari wakitumia mwanya huo kutoa elimu itasaidia ambao hawajajiunga kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokuingia.
Amesema vijana wengi wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na kuathirika na dawa za kulevya hali inayochangia nguvu kazi ya familia,Jamii na Taifa kwa ujumla kupungua.
“Dawa za kulevya huwa hazionjwi ukisha zionja tu basi tayari umeshajiingiza kwenye matumizi ya dawa hizo,hivyo nitoe wito kwa jamii,vijana kutojihusisha na matumizi ya dawa hizo,na endapo kwenye familia kunaviashiria vya ndugu yako vya kujiingiza kwenye dawa za kulevya mpeleke kwenye vituo husika ili aweze kupatiwa masaada wa dawa”,amesema Soko
Akizungumza wakati wa kufungua maadhimisho hayo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Thomas Rutachunzibwa amesema matumizi ya dawa za kulevya hudhoofisha afya ya mtumiaji na kusababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo homa ya ini,kifua kikuu na Ukimwi hasa kwa watumiaji kwa njia ya kujidunga na vifo vya ghafla.