WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inakusudia kupima utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu hususan usimamizi wa mapato na makusanyo ya ndani pamoja na upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema watendaji hao pia watapimwa kwa namna wanavyosimamia mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za ukaguzi zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 30, 2022) wakati akitoa Hoja ya Kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni jijini Dodoma. Amesema hatua hiyo ni katika kuhakikisha dhamira nzuri ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inayojiakisi kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 inafikiwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imejipanga vema kuendelea kusimamia suala la uwajibikaji katika utumishi wa umma kwa kuweka mikakati mbalimbali. “Mikakati ipo katika kuimarisha uwajibikaji hususan kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni pamoja na kupima utendaji wa utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara.”
Amesema mkakati mwingine ni kongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka shilingi bilioni 57.44 hadi shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hizo.
“Sambamba na ongezeko hilo la Bajeti katika mwaka 2022/2023, Serikali pia, imehuisha muundo wa Sekretarieti za Mikoa kwa kuboresha iliyokuwa Sehemu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa na kuwa Sehemu ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ili kuimarisha ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.”
Amesema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Madiwani, Mafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kupitia Programu ya Uimarishaji Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuongeza uelewa wa majukumu yao kisheria, kuimarisha mahusiano yao na viongozi wa kisiasa na kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kujenga mifumo na miundo wezeshi katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo. “Eneo hili linahitaji uwepo wa mifumo na miundo imara ambayo itawezesha kujenga msingi thabiti wa usimamizi wa utendaji kazi wa Serikali.”
Amesema hatua hizo zinajumuisha kupitia upya miundo na majukumu ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuziimarisha pamoja na kujenga uwezo wa watumishi katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya Sera ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuzihusisha taasisi simamizi zinazohusika na ufuatiliaji na tathmini ili kuchambua maeneo wanayosimamia na kuhakikisha maeneo yote muhimu yanajumuishwa ikiwemo usimamizi wa mipango ya maendeleo na utendaji wa Serikali kwa ujumla.
“Sambamba na hatua hizo, tayari, Serikali imekamilisha Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo ambao utaanza kutumika Julai, 2022. Mfumo huo, pamoja na mambo mengine utasaidia Serikali kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hivyo kuongeza tija na thamani ya matumizi ya fedha za umma kwenye miradi husika.”
Vilevile, Waziri Mkuu amesema Serikali imehuisha Muundo na Mgawanyo wa Majukumu wa Ofisi ya Waziri Mkuu hususan kwa upande wa Sera, Uratibu na Bunge ili kuimarisha jukumu la ufuatiliaji na tathmini. “Lengo ni kuhakikisha taarifa za ufuatiliaji na tathmini kutoka katika wizara na taasisi za Serikali zinafanyiwa uchambuzi wa kina pamoja na kutoa mrejesho kuhusu utendaji wa Serikali.”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha na Mipango kufanyia kazi changamoto ya uhaba wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini; kazi za tathmini kufanyika kwa ufanisi na uwepo wa mifumo mingi ya ukusanyaji wa taarifa yenye kuathiri ubora wa takwimu.
Amesema Serikali itaendelea kufanya tathmini ya ujuzi unaohitajika, kufanya tathmini ya mifumo ya ufuatiliaji na tathmini iliyopo kwenye taasisi za Serikali, kuandaa Kanzi-Data ya Watumishi wenye utaalamu wa masuala ya ufuatiliaji na tathmini, kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye ufuatiliaji na tathmini na kuimarisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini ili kujenga mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini ambao utawezesha kufuatilia, kuchambua na kupata taarifa halisi na kwa wakati za utendaji wa Serikali.