Muonekano wa daraja la Fundimbanga lililojengwa katika Mto Nanyungu wilayani Tunduru na wakala wa barabara za mjini na vijijni Tarura likiwa limekamilika.
Meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mhandisi Silvanus Ngonyani kushoto,akimsikiliza mkazi wa kijiji cha Fundimbanga Issa Lukoko alipokuwa akitoa pongezi kwa Serikali kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Fundimbanga.
Meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mhandisi Silvanus Ngonyani akikagua sehemu ya daraja la Fundimbanga.
Daraja la Fundimbanga kama linavyoonekana.
……………………………………
Na Muhidin Amri,Tunduru
WAKALA wa barabara mijini na vijijini(Tarura) wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,umekamilisha ujenzi wa daraja kubwa na la kisasa linalounganisha kijiji cha Fundimbanga,Matemanga na maeneo mengine ya wilaya ya Tunduru.
Meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Silvanus Ngonyani alisema,daraja la Fundimbanga limejengwa katika awamu kuu mbili na pamoja na barabara zake limeigharimu serikali jumla ya Sh.bilioni 1.456 na limekamilika kwa asilimia mia moja na limeanza kutumiwa na wananchi kwa ajili ya shughuli zao maendeleo.
Alisema,daraja hilo lina urefu wa mita arobaini na tano na upana wa mita nane na vivuko vya watembea kwa miguu kushoto na kulia mita moja moja na lina uwezo wa kubeba magari yenye uzito wa zaidi ya tani ishirini.
Alielezwa kuwa,kukamilika kwa daraja hilo kumemaliza kabisa changamoto ya madereva wa vyombo vya moto na wananchi kupoteza maisha kwa kutumbukia katika mto Nanyungu kipindi cha masika.
Ngonyani alisema,serikali kupitia wakala wa barabara mjini na vijijini(Tarura) inaendelea kutekeleza na kujenga miradi mbalimbali katika wilaya hiyo ili kuwezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa na mazao yao kwa urahisi katika kipindi chote cha mwaka.
Amewaomba wananchi,kulitunza daraja hilo na miundombinu yake ili liweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija iliyousudiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Wananchi wa kijiji cha Matemanga,Fundimbanga na Ligunga vinavyounda tarafa ya Matemanga,wameishukuru Serikali kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ambalo awali kulikuwa na daraja la miti, jambo lililohatarisha usalama wao na kurudisha nyuma uchumi wao.
Adam Omari mkazi wa Fundimbanga alisema,nyakati za masika maji yalifunika daraja hilo la miti hatua ambayo ilisababisha baadhi ya wananchi na vyombo vya moto kusombwa na maji na wengine kupoteza maisha.
Aidha alisema, hata wanafunzi wanaosoma shule ya Sekondari Matemanga wanaoishi kijiji cha Fundimbanga walilazimika kuzunguka umbali mrefu wakikwepa eneo hilo hatarishi.
Luka Luoga alisema kabla ya Tarura kujenga daraja, eneo hilo halikuweza kupitika kiurahisi, hivyo wananchi wa Fundimbanga na Matemanga walishindwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni na hivyo kutoa nafasi kwa walanguzi kwenda kununua mazao kwa bei ndogo.
Aliongeza kuwa,lakini baada ya kukamilika kwa ujenzi huo eneo hilo linapita kipindi chote cha mwaka bila usumbufu na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya kuboresha miundombinu ya barabara.
Naye Issa Lukoko mkazi wa Ligunga alisema,kujengwa kwa daraja hilo kumefungua mawasiliano katika kijiji cha Fundimbanga na tarafa yote ya Matemanga na kumechangia kasi ya ukuaji wa biashara kwa kuwa wakulima wengi wanapita katika daraja hilo kupeleka mazao yao mjini kwa ajili ya kutafuta masoko.
Alisema,katika kijiji cha Fundimbanga changamoto kubwa na ya muda mrefu ilikuwa kukosekana kwa daraja katika mto Nanyungu na walikuwa wakipata wakati mgumu kipindi cha masika hasa wanafunzi kuvuka kwenda upande wa pili,hali iliyopelekea wengine kuacha masomo ambapo ameipongeza Tarura kujenga daraja la kudumu.