****************************
Na Joseph Lyimo
KATIKA kipindi cha mwaka 2020 hadi hivi sasa maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 ulivyoingia nchini, mojawapo ya jambo ambalo jamii iliaswa kufanya ili kuepuka kupata maambukizo ya ugonjwa huo ni kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka, sabuni na vitakasa mikono.
Kutokana na hali hiyo wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, nao hawakuwa na budi ya kushiriki hilo kwa kuhakikisha wananawa mikono yao ili kujikinga au kujiepusha kupata maambukizo ya UVIKO-19.
Kila katika milango ya kuingia maeneo ya kwenye nyumba za kuishi, nyumba za ibada, soko na minada, mahoteli, shule za msingi na sekondari, ofisi za umma na taasisi binafsi ziliweka maji ambayo yalitumika kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kila mmoja anayetaka huduma au kuingia katika maeneo hayo.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt Damas Kayera anasema kuwa suala la wananchi kunawa maji kila wakati wanapoingia kwenye maeneo mbalimbali limebadili utamaduni na kuepusha magonjwa ya tumbo.
“Pamoja na miongozo ya maambukizi ya UVIKO-19 kitendo cha kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kwa mgeni na mwenyeji kwenye maeneo mbalimbali yamesaidia kuepusha magonjwa ya tumbo,” anaeleza Dkt Kayera.
Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendeleza utamaduni huo wa kunawa mikono yao mara kwa mara, kwani kwa kiasi kikubwa imechangia kuepusha maambukizi ya maradhi mbalimbali ya tumbo.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Dkt Aristidy Raphael anasema kuwa kutokana na wananchi wa eneo hilo kunawa kila mara kutokana na kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 kuliepusha magonjwa yote yanayoambukizwa kutokana na kula uchafu.
“Kipindupindu, magonjwa ya minyoo, kuharisha, magonjwa ya tumbo na mengineyo, yamepungua mno kutokana na jamii ya eneo hili kuwa na utamaduni wa kunawa mikono kila mara,” anaeleza Dkt Raphael.
Amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuendeleza usafi huo wa kunawa mikono yao kila wakati kwani hali hiyo inasababisha kuepuka maradhi hayo yanayotokana na kula uchafu.
Mchungaji Yohana Ole Tiamongoi anasema kuwa magonjwa ya kuhara yamepungua hivi sasa, kutokana na jamii kunawa mikono kila mara wakati wakijikinga na maradhi ya UVIKO-19 hivyo kuwa wasafi.
“Kunawa mikono imeonekana ni muhimu na siyo kuepuka na maambukizi ya UVIKO-19 pekee hata maradhi ya tumbo yamepata tiba kutokana na kunawa mikono kila mara kwa wananchi wa eneo hili la jamii ya wafugaji,” anazungumza Mchungaji Ole Tiamongoi.
Anasema kuwa wananchi walikuwa wananawa mikono kwa maji kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 ila magonjwa mengine yalikuwa yanawanyemelea kutokana na kutokunawa ila usafi umesaidia watu na kutambua kwamba kunawa ni muhimu tofauti na hapo awali.
Anaeleza kwamba kitendo cha kunawa mikono kwa maji kwa jamii ya wafugaji imekuwa ni msaada wa kuepuka maradhi mengine ambayo yalisababishwa na kutokunawa kwani maeneo haya ya wafugaji inaonekana ni sehemu yenye maradhi mengi ya tumbo.
Mfamasia na mmoja wa wakurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Jamii Yangu Begani, Lowassa Laizer anasema unawaji mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka siyo tu umekinga maambukizi ya UVIKO-19 ila na maradhi mengine yanayosababishwa na uchafu.
“Jamii ya eneo hili la Simanjiro iliepuka kupata magonjwa ya milipuko kama kipindupindu, kuharisha na homa ya matumbo japokuwa wengine wanaoishi kwenye nyanda kame walikuwa na wakati mgumu wa kupata maji,” anaeleza Lowassa.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Orkiringo, Kijiji cha Narakauo, Kata ya Loiborsiret, Wilayanin Simanjiro, Mosses Ole Sanjiro, anasema muongozo wa kutokuingia sehemu bila kunawa mikono kwa lengo la kuepuka maambukizi ya UVIKO-19 kwa namna moja au nyingine ilisaidia hali ya usafi na kuondokana na maradhi mengine.
Ole Sanjiro anaeleza kuwa jamii na wanafunzi walibadilika mno kwani walikuwa wananawa mikono hata mara 10 kwa siku moja hivyo kupata somo la usafi kwa njia ya vitendo.
“Jamii ilipata elimu ya kunawa na kusababisha magonjwa ya watoto wadogo yanayosababisha kuhara wakati wa kutambaa yalipungua mno kama siyo kumalizika kabisa eneo hilo,” anaeleza Ole Sanjiro.
Mfugaji wa kijiji cha Naberera, John Martin akiUmgumza juu ya hilo anasema UVIKO-19 pia ilisababisha upendo kupungua kwa baadhi ya watu waliozoea kusalimiana kwa kushikana mikono ila kutokana na hofu ya maambukizi watu wamebaki kupungiana.
“Misikitini na Makanisani hivi sasa watu hawapeani mikono tena kutokana na hofu ya maambukizi ya UVIKO-19, kwani wanapungiana mikono tuu hata kama wapo karibu, wakitekeleza maelekezo ya wataalamu wa afya,” anamalizia Martin.