*************************
Ni katika kilele cha maonesho ya mabahari duniani ambapo serikali imeahidi kuwapambania mabahari katika maslai yao na kuwafanya wanufaike katika kazi yao.
Kauli hivyo imetolewa na katibu tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora ambae alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya waziri wa ujenzi na uchukuzi katika siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mayunga Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera juni 25, 2022.
Prof Kamuzora amesema kuwa serikali kupitia TASAC wameendelea kushirikiana vyema ili kuboresha mazingira ya mabaharia ambapo amesema serikali imeendelea kuwajali mabaharia kwani tayari imeamua kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 23.1, kulinda haki za mabaharia, afya, mazingira bora ya kufanyia kazi, huduma za matibabu na utaratibu wa mabaharia kuwasilisha malalamiko endapo baadhi ya vipengele vinapokiukwa ikiwemo kutatua changamoto zao.
Amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TASAC na chuo Cha bahari(DMI) wameendelea kufanya mazungumzo na kampuni moja kubwa kwa ajili ya mabaharia kupata mafunzo maalum, ambapo TASAC imeendelea kuboresha huduma za kutoa vyeti, ambapo wanatumia siku 3 kuhakiki cheti, kusimamia ubora wa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika vyuo ili kufanya mmabaharia kuwa na ujuzi wenye viwango vinavyokubalika ndani na nje ya nchi.
Katibu tawala huyo ameongeza kuwa serikali kupitia TASAC wameendelea kushirikiana na wizara ya ujenzi na uchukuzi na ofisi ya takwimu ya taifa wizara ya mifugo na uvuvi kwa kufanya sensa ya vyombo vya majini nchi nzima ili kuwatambua mabaharia wadogo wadogo wanaoendesha vyombo vya majini kwa lengo la kupata fursa za mafunzo yatakayowasaidia kuwa na vyeti na kufanya kazi kwa weledi.
“Sekta ya usafiri wa majini ina fursa kubwa hivyo niwahimize wananchi Mkoani Kagera na watanzania kwa ujumla kujenga hali ya kujifunza elimu ya ubaharia na kuenzi mabaharia.
Naye Bi Josephine Bujiku kaimu Meneja masoko na uhusiano wa TASAC amewashukuru washiriki wote kutoka Tanzania bara na visiwani na wenyeji Kagera kwa maadalizi makubwa ya tukio hilo huku akitaja shughuli zilizofanyika ikiwemo zoezi la kuonyesha kwa vitendo namna ya uokoaji katika ajali au inapotokea dhoruba majini.
Pia washiriki kutoa elimu ya usalama wa usafirimajini kwa wanafunzi ikiwemo kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya fani ya ubaharia ambapo jumla ya wanafunzi 4,200 kutoka shule za sekondari Mkoani Kagera ikiwemo shule ya sekondari Rugambwa, Bukoba, Kahororo na Ihungo wamenufaika na elimu hiyo.
Bi Bujiku ameongeza kuwa elimu hiyo itaongeza hamasa kwa watanzania na wananchi Mkoani Kagera kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya usafiri wa majini.
Kwa upande wa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TASAC Capten Mussa Hamza Mandia amesema mabaharia ni nguzo kubwa kiuchumi na kuwa nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya maji hivyo vitumike vyema na kuwa TASAC wanalenga kutembelea maeneo mengi zaidi ikiwemo kukagua miundo mbinu yake na usalama wa raia ikiwemo kutoa elimu zaidi juu ya ubaharia.