Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe akipokea ripoti ya Sensa ya Viwanda vya Kusindika Vyakula kutoka kwa o ni Mwakilishi Mkazi wa shirika la WFP Sarah Gordon.
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe akionesha ripoti ya Sensa ya Viwanda vya Kusindika Vyakula ilifanywa na Shirika la WFP, kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa shirika hilo Sarah Gordon
**********************
Na Mwandishi Wetu
ASILIMIA 90 ya viwanda 33,000 vya kusindika vyakula vilivyofanyiwa sensa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) vimebainika kutoweka virutubishi.
Hayo yamesemwa mwisho mwa wiki jijini Dodoma na Mwakilishi Mkazi wa WFP nchini, Sarah Gordon wakati akikabidhi ripoti ya sensa ya wamiliki wa viwanda vya kusindika vyakula kwa Naibu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.
Gordon alisema viwanda vingi vinavyosindika vyakula vina mashine za zamani, hali ambayo inakwamisha kuweka virutubishi muhimu kwenye vyakula vya binadamu.
“WFP tulifanya sense kwenye viwanda 33,000 ambapo zaidi ya asilimia 90 ya viwanda hivyo haviweki virutubishi muhimu, hali ambayo inaondoa msingi mzuri wa kuboresha afya za wananchi hasa watoto,” alisema.
Mwakilishi huyo alisema katika sense hiyo walibaini kuwa viwanda vingi vinamilikiwa na watu wenye miaka kuanzia 36 hadi 55, huku asilimia 7 ya mashine hizo zinamilikiwa na wanawake.
Alisema katika viwanda hivyo vya kusindika vyakula kuna wafanyakazi 1,091 ambapo asilimia 25 ni wanawake na 75 wanaume, huku wamiliki wengi wakiwa ni sekta binafsi.
“Pia sensa hii imebaini katika viwanda hivyo 33,000 asilimia kubwa vinazalisha vyakula vya mahindi, na vinatumia nishati ya umeme kama nyenzo muhimu ya uzalishaji,” alisema.
Mwakilishi huyo alisema WFP Tanzania imefanya sensa ya kina kuhusu viwanda vya ngano na viazi ili kuwa na taarifa sahihi na nafasi ya mazao hayo, yanapopatikana, usambazaji wake, kiasi, virutubishi na uhitaji.
Gordon alisema lengo ni kuhakikisha usalama na lishe inakuwepo kwenye chakula hapa nchini, huku akiweka bayana kuwa WFP Tanzania imefanikisha zoezi hilo kwa taasisi ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ) kwa kusimamiwa na Kitengo cha Lishe na Ubunifu.
“Sensa hii iligawanyika katika sehemu tatu ambapo mosi ilikuwa ni kuzunguka kwenye viwanda, kufanya kazi, na kukusanya taarifa, ambapo zoezi limeenda vizuri hadi leo tunatoa ripoti hii, muhimu kwa afya na maendeleo ya jamii,” alisema.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Naibu Waziri Kigahe alisema imesaidia kutoa takwimu ambazo zitakuwa muongozo kwa Serikali kujua pa kuanzia katika eneo hilo la virutubisho.
Naibu Waziri alisema pia ripoti hiyo inatoa picha sahihi ya idadi ya ajira zilizopo kwenye viwanda hasa vya kusindika vyakula na kwanini haviweki virutubishi.
“WFP wamefanya jambo muhimu sana kwani ni dhahiri kuwa kwa sasa tunamwanga kuhusiana na hali ya uwekeji virutubishi kwenye vyakula, ila pia ajira, teknolojia na mengine ambayo yanahusina na sekta hiyo ya viwanda,
alisema.
Alisema Serikali itakuwa inachukua hatua awamu kwa awamu ili kuhakikisha sekta hiyo inafankiwa kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo nchini.