Na Catherine Mbena-ARUSHA
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka ameelekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuhakikisha hifadhi zote ambazo bado ni tegemezi zinafikia uwezo wa kujiendesha ndani ya mwaka 2022/2023 alipotembelea makao makuu ya shirika hilo jijini Arusha leo 25.06.2022.
Prof. Sedoyeka alisema “kazi ya uhifadhi mnaifanya kwa mafanikio makubwa sana hivyo juhudi hizi zionekane kwenye mapato yanayotokana na shughuli za utalii. Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya kwani maoni ya watalii na tuzo mbalimbali ambazo mmepata ni ishara tosha kwamba mnafanya kazi nzuri sana.”
Amesisitiza kwamba shirika linatakiwa kutangaza utalii wa ndani na kuhakikisha linakuwa na maeneo ya kutosha ya malazi na sehemu nzuri za huduma ya chakula kwa ajili ya watalii wa ndani.
Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa, William Mwakilema aliwasilisha taarifa fupi kuhusu TANAPA na majukumu yake na kubainisha kuwa watalii wameanza kuja kwa wingi.