Kiongozi msaidizi wa Kituo cha WISE-Futures, Dkt. Yusufu Chande Jande (kwanza kushoto), Afisa Viwango TBS, Bw.Arnold Mato( wa pili kulia), Afisa Sheria TBS , Bi. Lucy Mallya, wakitoa elimu ya vichuja hewa kupitia radio Kicheko FM ya Moshi mjini.
…………………………………………….
Na Elizabeth Mushi,Arusha
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, kupitia Kituo cha Umahiri cha Miundombinu ya Maji na Nishati endelevu (WISE-Futures), kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamefanya ziara katika vyombo vya habari vya radio kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa upimaji wa ubora wa chujio za hewa (airfilter) kwenye magari.
Akizungumza katika ziara hiyo iliyoanza Juni13, hadi Juni 25, 2022, Kiongozi msaidizi wa Kituo cha WISE-Futures, Dkt. Yusufu Chande Jande amesema kuwa, machujio ya magari yasipokuwa na ubora unaotakiwa huathiri magari kwa kuharibu injini ya gari, kutumia mafuta mengi na kuleta athari za kiafya na mazingira.
Kwa upande wake Afisa Viwango wa TBS, Bw. Anorld Mato, alisema kuwa wanashirikiana na NM-AIST kupima ubora huo kutokana na Taasisi hiyo kuwa na maabara ya kisasa ambapo kwa upande wa TBS imeandaa viwango vya ubora wa machujio hayo na kusimamia jukumu la hakikisha ubora wa bidhaa hizo unafatwa.
Alibainisha kuwa, viwango vya upimaji wa machujio hayo ya aina mbili, kiwango cha TZS 3208 cha mwaka 2021 ikiwa ni chujio za kuchuja hewa ya AC, kiwango cha TZS 1959 cha mwaka 2018 ambacho huchuja hewa inayoingia kwenye injini ikiwa ni viwango vya lazima katika bidhaa hizo.
Aidha, Bw. Mato ametoa wito kwa watumiaji wa bidhaa hizo, kutumia machujio bora kwa usahihi kwa kuzingatia muda uliowekwa wa matumizi, kuangalia alama ya ubora iliyowekwa kwenye bidhaa ili kulinda afya zao.
Naye Afisa sheria wa TBS, Bi, Lucy Mallya, amewataka watengenezaji na waagizaji wa bidhaa hizo kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa na kufuata sheria zilizopo ili kuepuka adhabu endapo wataenda kinyume na sheria, ikiwepo kurudisha bidhaa kwa nchi iliyotengeneza au kuziharibu bidhaa hizo kwa gharama za muagizaji.
Mnamo Juni 08, 2021, NM-AIST na TBS waliingia makubaliano ya upimaji ubora wa machujio ya magari ili kudhibiti na kusimamia ubora wa chujio za hewa na magari zinazozalishwa ndani na nje ya nchi , ikiwa ni hatua ya kuzingatia afya za watumiaji wa bidhaa hizo hapa nchini.
Shirika la viwango Tanzania (TBS) ikishirikiana na NM-AIST imekuwa ikitoa huduma ya upimaji ubora wa machujio ya hewa kwa kutumia mtambo wa (air filter tester machine) ambao unapatikana katika maabara ya NM-AIST, Kutumia mtambo huo ambao ni wa aina yake na pekee nchini Tanzania umekuwa ukipima ubora wa chujio za hewa ya magari (AC) na machujio za hewa inayoingia kwenye injini za magari ambazo zinazozalishwa hapa nchini na zinazoagizwa nje ya nchi kwa kupima ubora wa chujio zote za hewa ya magari ili kuona kama zinakidhi viwango vilivyowekwa.