************************
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro ameendelea kulaani vitendo vya mauaji vinavyofanywa na baadhi ya watu kwenye jamii na kamwe vitendo hivyo haviwezi kuvumiliwa na kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
IGP Sirro amesema hayo akiwa mkoani Iringa ambapo kabla ya kuzungumza na wadau mbalimbali wa Jeshi hilo alikagua gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili yake na pia kukagua mazoezi ya mbinu za medani.
Kuhusu matukio ya makosa ya ubakaji na makosa ya kijinsia IGP Sirro ameutaja mkoa wa Iringa kama kinara wa makosa ya ubakaji na makosa ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na imani za kishirikina.
Aidha, IGP Sirro ameendelea kusisitiza suala la ulinzi wa umma na kwamba wananchi wanatakiwa kushiriki kwenye jukumu la ulinzi na vikundi vya ulinzi shirikishi.
Kuhusu suala la maadili IGP Sirro amewataka askari wa Jeshi hilo kuheshimu Watanzania na kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi wanaowahudumia.