Mhashamu Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida akiongea na waumini na wananchi wa kijiji cha Mvae wakati wa adhimisho la Misa takatifu ya Katekista Mzee Patrisi kumshukuru Mungu kwa kutimiza umri wa karne moja ambayo ni sawa na miaka 100 iliyofanyika Juni 09, 2022 katika Kigango cha Mvae Parokia ya Ilongero jimboni humo.
Padre Castor Kisuda wa Shirika la Roho Mtakatifu ambaye pia ni mjukuu wa Katekista Mstaafu Mzee Patrisi Paulo Mangi akitoa homilia wakati wa adhimisho la Misa takatifu ya Katekista Mzee Patrisi kumshukuru Mungu kwa kutimiza umri wa karne moja ambayo ni sawa na miaka 100 iliyofanyika Juni 09, 2022 katika Kigango cha Mvae Parokia ya Ilongero Jimbo Katoliki la Singida.
Mhashamu Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida akibariki miti mitatu ya mizeituni ambayo imepandwa kwa ajili ya kumbukumbu ya Katekista Mstaafu Mzee Patrisi Paulo Mangi kwa kutimiza umri wa karne moja ambayo ni sawa na miaka 100.
(Picha na Eleuteri Mangi)
**********************
Na Eleuteri Mangi
“Chanda chema huvikwa pete” ni msemo wa Kiswahili unaosadifu maisha mazuri ya mtu na wema anaoufanya kwa watu wengine na Mwenyezi Mungu humjalia mtu huyo neema katika ulimwengu kwa wema alioufanya kwa watu wake.
Katekista Mstaafu Mzee Patrisi Paulo Mangi wa Kigango cha Mvae kutoka Parokia ya Ilongero Jimbo Katoliki la Singida anasadifu msemo huo ambapo Juni 09, 2022 amedhimisha Jubilei ya karne moja ambayo ni sawa na miaka 100 tangu kuzaliwa kwake mwaka 1922, huku akisema “Yeye ni Mwana wa Mungu.”
Ibada ya Misa takatifu ya kumshukuru Mungu kwa Mzee Patrisi kwa kutimiza umri huo ambayo ilifanyika nyumbani kwa Katekista huyo katika Kigango cha Mvae na kuongozwa na Askofu Mhashamu Edward Mapunda ameungana na waumini na wanchi waliofurika nyumbani hapo amesema Jimbo linampongeza Katekista Mzee Patrisi kwa kutimiza umri wa karne moja na kufananisha maisha yake na mti mzuri .
“Mti mzuri Yesu ametuambia unatambulikana kwa matunda yake, mzee Patrisi ni mti mzuri katika kanisa uliotambulikana kwa matunda yake mazuri, hongera sana Mzee, Jimbo Katoliki Singida linaungana nawe kumpa Mungu sifa na shukrani” amesema Askofu Mapunda.
Askofu Mapunda amemshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, imani ya kikristo, utume wa Ukatekista na pia utume wa familia aliyomjalia Mzee Patrisi na kusisitiza kumrudishia Mungu sifa na shukrani.
“Mzee Patrisi ni kielelezo cha namna sisi sote tunavyopaswa kuishi imani yetu ya kikristo, kama tulivyosikia katika historia ya maisha yake, alivyokuwa na bidii kubwa, ari kubwa na ujasiri mkubwa wa kuishi imani yake na kutushirikisha sisi sote imani ambayo Mungu alimjalia” amesema Askofu Mapunda.
Askofu Mapunda ameongeza kuwa Mungu hatuajalii tu imani, bali anatujalia imani hiyo kwa ajili ya taifa lote la Mungu, Mzee Patrisi ni kielelezo bora cha maisha ya imani na kielelezo bora cha maisha ya familia.
Akinukuu maneno ya Mzee Patrisi alipokuwa akiwakaribisha wageni nyumbani kwake wakati wa Ibada ya Misa takatifu alisema yeye ni mwana wa Mungu, Askofu Mapunda alisema sisi sote tunapswa kuishi hivyo maana baada ya kubatizwa tunafanywa wana wa Mungu.
Kwa hiyo mzee ni mwalimu wa imani yetu, hakika ni mwalimu wa maisha ya Kikristo, yeye ni nyota ambayo inatuongoza namna ya kuishi maisha ya Kikristo na amewahimiza watu wote kufundisha dini kuanzia ngazi ya familia ili kanisa liendelee kustawi na kukuza miito katika kanisa.
Aidha, Askofu Mapunda ametumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini kuwa mwaka wa 2022 Jimbo hilo linaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972 likiongozwa na Askofu mwanzilishi Hayati Mhashamu Bernard Mabula na baadaye chini ya Askofu wa pili Mhashamu Desderius Rwoma ambaye sasa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba.
Akionesha mchango wa Mzee Patrisi katika kanisa Askofu Mapunda amesema Katekista huyo ni miongoni mwa wazee wa jimbo hilo ambao waliandaa kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki Singida katika mambo ya imani, mambo ya dini na kuwa zawadi kwa majitoleo yao kwa kanisa huku akiwashukuru wanafamilia kwa kumtunza mzee vizuri kama Amri ya nne ya Mungu anavyohimiza “Waheshimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani”.
Awali akiwakaribisha wageni nyumbani kwake wakati wa Ibada ya Misa takatifu Mzee Patrisi Paulo Mangi alisema anawakumbuka, anawapenda watu wote kwa kuwa tangu akiwa mtoto mdogo alikuwa anawapenda watu na sio kugombana.
“Leo namshukuru sana Baba Askofu aliyenikumbuka maisha yangu, nimezaliwa mwaka 1922 na nimeingia kwenye dini mwaka 1946 sasa ni mzee wa kikristo, sina mambo mengi mimi najua Baba Askofu na mapadre ni watu wenye ngao kubwa ya kuchunga kondoo wa Mungu” amesema Mzee Patrisi.
Akinukuu maneno matakatifu Mzee Patrisi alisema “Yeye alisema enendeni ulimwenguni kote mkawafundishe wote (Mk 16:15) na kuongeza kuwa yeyote anayewakubali ninyi ananikubali mimi, wanaowachukia ninyi, wananichukia mimi na Baba yangu na kusisitiza Kristo aliwadhihirishia wanafunzi wake kuwa mimi nipo pamoja nanyi siku zote (Mt 28:20).
“Mimi maisha yangu yote ni kufuata wakubwa, sasa mimi nawafuata watu hawa ni wakubwa wangu, Maaskofu, mapadre, mashemasi, mafrateri na masista, ni wakubwa maana wamechukua kitu kikubwa wanafanya kazi bora katika uhai wa roho zetu. Sina mengi karibuniu wote katika jubilei hii ya mwana wa Mungu” amesema Mzee Patrisi.
Katika homilia ya ibada hiyo ambayo ilitolewa na Padre Castor Kisuda wa Shirika la Roho Mtakatifu ambaye pia ni mjukuu wa Mzee Patrisi amesema maadhimisho ya ibada hiyo ya misa takatifu ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa uhai ambayo ni maisha ya mjubilei Patrisi, imani na utume wake wa kulitumikia kanisa na taifa la Mungu akiwa Katekista.
Padre Kisuda amesema kuwa katika ibada ya neno Mt. Paulo katika barua yake kwa Wakolosai anawaalika waumini kuvaa mavazi ya upole, uvumilivu, unyenyekevu, upendo na kusameheana ambayo ni mambo muhimu katika maisha ya familia, baba, mama na watoto na ambapo kila mwanafamilia anapswa kutimiza wajibu wake.
“Mapadre wenzangu, kazi ya uchungaji wetu ni ngumu hasa kuzilea hizi familia za Mungu ambazo tunaziongoza na kondoo wetu, ni waumini wetu, hakika maisha ya famia ni changamoto katika maisha ya sasa’,
‘Unaweza kufanya kazi yako ya kichungaji vizuri, ukawa na kwaya nzuri inaimba kweli lakini ukakuta ni watu waliovunjika mioyo kwa sababu ya uzito wa maisha ya familia wanayopitia” ameongeza Padre Kisuda.
Padre Kisuda ameongeza kuwa Mzee Ptrisi amekuwa katekista kwa muda mrefu ambapo moja ya kazi aliyokuwa akiifanya ni kujenga familia kuandaa watu kwa ajili ya maisha ya ndoa na ni kazi ambayo walikuwa wanaifanya kwa umakini sana.
“Hizi familia ni kanisa, kama hazijaungana vizuri, kama hazisali pamoja, hazina kusameheana, hazina upendo, ni hatari kanisa tunaweza kuwa kama mashabiki kwenye uwanja wa mpira wote tunashangilia” amesema Padre Kisuda.
Akitoa ushuhuda katika kazi yake ya kichungaji, Padre Kisuda anasema akiwa nchini Zambia alifanya utume wake nyumba kwa nyumba na Ofisi yake ilikuwa ni nyumba za watu hata wakati wa usiku wa manane nilienda kwa waumini kwa sababu wengine walikuwa na visingizio wapo kazini. Nilijikuta naijua Parokia nzima kitu ambacho kwake ilikuwa faraja kwa kuwa aliwajua watu aliokabidhiwa na kufanya nao kazi.
Padre Kisuda amesema katika maadhimisho mbalimbali ya ibada watu wengi hawapokei sakramenti kwa sababu ya vizuizi walivyonavyo, Mzee Patrisi amewaita watu wote nyumbani kwake, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuonja mapendo hayo na kutafakari ni namna gani anaweza kujenga na kuwa nafuraha katika familia yake.
Wasifu wa Mzee Patrisi Paulo Mangi
Mzee Patrisi amezaliwa mwaka 1922 katika kijiji cha Matongo sasa Mvae na wazazi Paulo Mangi na Mama Katarina Soghweda akiwa mtoto wa pili kuzaliwa kati ya wataoto 10 huku miongoni mwa wadogo wake akiwa Padre Thomas Mangi Jimbo Katoliki Singida.
Mzee Patrisi ni baba mzazi wa Padre Patern Mangi Jimbo Katoliki Singida na Paroko wa Parokia ya Mt. Joseph Mfanyakazi Mandewa iliyopo manispaa ya Singida pia ni baba wa Sista Dkt. Sabina Mangi wa Shirika la Masista wa Teresina Jimbo katoliki la Iringa.
Mzee Patrisi alianza mafundisho ya dini Katoliki na kubatizwa Mei 25, 1948 katika Parokia ya Itamka sasa Ilongero iliyokuwa chini ya Mapadre wa Shirika la Palotine. Alifunga ndoa na Mama Teresia Bonifansi Desemba 29, 1948 parokiani Itamka ndoa ambayo ilidumu kwa miaka 70 hadi Mungu alipomwita Mama Teresia kwake Novemba 9, 2017.
Kwa upande wa elimu, Mzee Patrisi alihamasishwa kusoma na babu yake Mzee Kimu ambaye alirudi kutoka kupigana vita vya II vya Dunia 1945 ambapo alimpatia zawadi ya kitabu cha kusoma na kuandika hatua iliyomsukuma apende kuwafuata walimu na kumfanya ajifunze kusoma na kuandika ambapo hadi sasa anaweza kusoma, kuandika na kuhesabu kwa ufasaha, hakika hiyo ni elimu ya aina yake.
Utume katika Kanisa Katoliki
Mwaka 1946 Mzee Patrisi alifanya utume katika Aksio Katoliki na kuwa Katekista na Mwalimu Msaidizi wa Katekista Thadei katika kanisa la Kitamjigha. Mwaka 1957 alichaguliwa kuwa Katekista katika kigango cha Matongo (sasa Mvae) hadi alipostaafu mwaka 1991.
Katika utume wake alipenda kuwaendeleza na kuwatia moyo vijana katika utume wa kanisa ambapo wengine walijiunga na seminari akiwemo mdogo wake Padre Thomas Mangi na wengine kujiunga na utawa wa kike na wa kiume. Kwa watoto wa kike wapo aliyewapeleka nyuma ya kitawa ya Mgolole mkoani Morogoro na kituo cha malezi cha Makiungu na wenginge kujiunga na miito na kuishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Aidha, juhudi zake za kupenda kazi ya Mungu zilisaidia kueneza dini Katoliki eneo la Wirwana ambayo ni Singida Kaskazini. Vigango vilivyozaliwa na Kigango cha Mvae ambacho kilisimamiwa na Mzee Patrisi ni Mdilu, Merya, Ghata, Msimihi, Msange, Mangida, Itaja na Ngamu. Minongoni mwa vigango hivyo zimezaliwa Parokia mbili za Itaja na parokia teule ya Laghanga.
Uongozi katika Serikali
Mzee Patrisi ameshika pia madaraka katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ambapo mwaka 1954 alichaguliwa kuwa Katibu wa chama cha TANU tawi la kijiji cha Matongo kwa sasa ni Mvae na Machi 19, 1973-1978 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho.
Katika utendaji kazi wake uliotukuka, Mzee Patrisi pamoja na kustaafu kwake utume wa kanisa na Serikali, ameendelea kuwa mshsuri mzuri katika kanisa na serikali. Amewaongoa watu wengi ikiwemo famila ya baba yake, ndugu, jamaa na marafiki katika kijiji cha Mvae na eneo la kanda ya Wirwana ambayo ni Singida Kaskazini kuwa Wakristo wakatoliki.
Shughuli za Maendeleo
Akiwa Aksio Katoliki yeye pamoja na viongozi wenzake walijadili na kuona eneo la Wairwana halikuwa na shule miongoni mwa vijiji hivyo ni kijiji cha Mvae. Hivyo, uongozi huo ulipeleka maombi kwa Mkuu wa Wilaya (DC) wakati huo ambapo maombi yao yalikubaliwa na hivyo kuanzishwa shule ya msingi Mvae amabyo ilianza kujengwa mwaka 1952 na kufunguliwa rasmi mwaka 1954.
Hakika nyota yake ya uongozi ilig’ara wakati wa uongozi wake kwa kuleta maendeleo kijijini hapo ambapo mwaka 1974 akiwa Mwenyekiti wa kijiji alitambua adha na madhila waliyokuwa wanapata wananchi wake juu ya maji, hivyo alianzisha mradi wa kusambaza maji kijijini hapo kwa kushirikiana na Idara ya Maji Singida kwa kuandaa miundombinu ya maji ambayo inatumika hadi sasa kutoa huduma ya maji kwa wananchi kulingana na maeneo yao.
Zaidi ya hayo, Mzee Patrisi alikuwa mtunzaji wa mazingira kwa kutunza miti ya asili katika mashamba yake na maeneo yanayozunguka mji wake ambayo miti mingine bado ipo hadi sasa.
Hakika kanisa ninajivunia kazi njema inayofanywa na Makatekista katika kuwafundisha watu wa Mungu dini ambayo ndiyo inawaunganisha wanadamu na muumbao wao.
Katekista Patrisi yeye ni tunda la kanisa alizaliwa kiroho na kufanywa kuwa mwana wa Mungu (Yohana 1:12-13) na yeye akiwakaribisha wageni kwenye ibada amekiri kuwa jubilei yake ni ya mwana wa Mungu kwa kuwa alizaliwa kwa mapenzi na kusudi lake Mungu mwenyewe kutimiza wajibu aliopewa hapa duniani.