Aliyeshika kombe mwenye kofia ni Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Arusha,Prof.Patric Manu akimkabithi mmoja wa washindi kombe ,aliyeko katikati ni Mkurugenzi wa fedha na uhasibu kutoka chuo hicho ,Yusuph Zegge .
……………………………………………..
Julieth Laizer , Arusha
Chuo kikuu cha Arusha kimepata Timu ya kuwawakilisha katika mashindano mbalimbali baada ya Timu ya kitivo cha elimu mwaka wa tatu kuibuka kidedea na kupata alama 13 dhidi ya Timu ya kitivo cha elimu ya theolojia ambao wamepata alama 12.
Akizungumza wakati wa ligi ya Makamu Mkuu wa chuo hicho ambayo ilishirikisha timu sita chuoni kwa lengo ya kupata timu hiyo, Makamu Mkuu wa chuo hicho,Prof Patric Manu amesema kuwa, lengo la kuanzisha ligi hiyo ni ili kupata mwakilishi katika mashindano mbalimbali ikilinganishwa kuwa chuo hicho ni kikubwa.
Amesema kuwa,hapo awali kulikuwa na timu lakini waliokuwepo walishahitimu masomo yao ambapo kila mwaka watakuwa wanachagua timu ambayo itakiwakilisha chuo hicho katika michezo mbalimbali.
Prof. Manu amesema kuwa, uwepo wa michezo vyuoni ni muhimu Sana kwani inasaidia kuwaondolea wanafunzi msongo wa masomo pamoja na kufanya mazoezi kwa lengo la kuimarisha afya zao.
“Mimi nitaendelea kufadhili timu hii ili iweze kuwa timu bora zaidi ambayo itaweza kutuwakilisha maeneo mbalimbali, na natoa wito kwa vyuo vingine kuhakikisha wanakuwa na utaratibu huo na uwe endelevu pia.”amesema Prof .Manu
Naye Mkurugenzi wa fedha na uhasibu ,Yusuph Zegge amesema kuwa,ligi hiyo ilishirikisha vitivo vyote vya chuo hicho ambapo imefanyika kwa muda wa wiki mbili na hatimaye kuweza kupata mshindi.
Amesema kuwa, uwepo wa michezo vyuoni unasaidia wanafunzi kujenga mahusiano na wakufunzi wao ,na wakati mwingine kuweza kuondokana na magonjwa nyemelezi .
Zegge amesema kuwa, wameweka mikakati ya kuhakikisha wanafufua timu ya wanawake iliyokuwepo chuoni hapo ili iweze kupewa kipaumbele na kushiriki katika michezo mbalimbali ya wanawake na kuweza kukitangaza chuo hicho.
Kwa upande wake ,Mdau wa michezo ,Joel Kasindi alikipongeza chuo hicho kwa kuanzisha ligi na kuweza kupata timu hiyo ambayo itawawakilisha katika mashindano mbalimbali na hatimaye kuweza kupata vijana ambao mwisho wa siku watakuwa wachezaji bora na wa kimataifa kama walivyo wengine.
Kwa upande wa kocha wa Timu hiyo iliyoshinda , Andrew Elias amesema kuwa,ushindi huo umetokana na kujiandaa vizuri kwa timu hiyo na mikakati waliyojiwekea.