Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akitoa maelekezo kwa mkandarasi anayejenga Daraja la Nyeburu Mhandisi Mussa Miraji wa kampuni ya Giraf Investment kuhakikisha daraja hilo linalounganisha Pugu na Chanika linakamilika kwa wakati. (Pembeni ni mhandisi matengenezo wa TANROADS mkoa wa Dar es salaam Eliseus Mtenga )
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa mhandisi matengenezo wa TANROADS mkoa wa Dar es salaam Eliseus Mtenga wakati aliposimama katika Daraja linalojengwa la Nyeburu linalounganisha Pugu na Chanika leo tarehe 17 Juni 2022.
**************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa wakandarasi wazawa kutumia vema na kwa ufanisi fursa wanazopewa na serikali za ujenzi wa miradi mbalimbali ili kuendelea kupewa nafasi hizo zaidi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati aliposimama na kukagua ujenzi wa daraja la Nyeburu linalounganisha eneo la Pugu na Chanika Jijini Dar es salaam ambalo ujenzi wake umekuwa ukisuasua. Makamu wa Rais ameonesha kutofurahishwa na maendeleo ya ujenzi huo ambapo amaesema ujenzi wa daraja hilo umechukua muda mrefu na kutoa athari kwa wananchi hasa wakati wa mvua licha ya serikali kuendelea kutoa malipo kwa wakati kwa mkandarasi katika kila kazi.
Aidha Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani kutokana na kutambua wanafahamu vema changamoto zinazosababishwa na ubovu wa miundombinu hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kiufanisi zaidi.
Pia Makamu wa Rais amewataka wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) pamoja na TANROADS kuwasimamia kikamilifu wakandarasi ili wakamilishe miradi kwa wakati na kuokoa fedha za walipa kodi wa Tanzania.