TIMU ya Yanga SC imekamilisha mechi zake Yanga za kujipima nguvu katika kambi yake ya Mwanza kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Toto Africans jioni ya leo Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
Ushindi huo umetokana na mabao ya mshambuliaji mpya, David Molinga ‘Falcao’ aliyefunga mawili dakika ya 37 na 41 na kiungo mpya pia, Mzanzibari Abdulaziz ‘Bui’ Makame dakika ya 51.
Na ushindi huo unafuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo uliopita dhidi ya timu nyingine ya Daraja la Kwanza, Pamba SC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, bao la Yanga likifungwa na Molinga pia.
Baada ya mchezo huo, Yanga SC wanatarajiwa kupanda ndege kurejea Dar es Salaam tayari kuwakabili Zesco United Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa wiki yote hii Yanga SC wamekuwa mjini Mwanza kujiandaa na mchezo wa kwanza na Zesco United ambao viingilio vyake ni; Sh 100,000 Royal, Sh. 25,000 VIP A, Sh. 10,000 VIP B na C na 3,000 Orange, Blue na Green.
Kikosi cha Toto Africans kilikuwa; Samuel Simon, Petro Bundala, Geoffrey Joshua, Said Ngoma, Joshua Bundala, Shaibu Gaddafi, Samanyi Kihamba, Madinda Maichael, Saleh Abdul, Didas Msafiri na Abdul Mkono.
Yanga SC; Metacha Mnata, Mapinduzi Balama/Deus Kaseke dk46, Ally Mtoni ‘Sonso’/ Muharami Issa dk46, Ali Ali/ Moustafa Seleman dk46, Lamine Moro/ Said Juma ‘Makapu’ dk46, Abdulaziz Makame, Mrisho Ngassa/Jaffar Mohammed dk46, Raphael Daud/Issa Bilali dk46, David Molinga/ Melbin Kalengo dk46, PapyKabamba Tshishimbi/ Faisal Salum ‘Fei Toto’ dk46 na Sadney Urikhob/ Juma Balinya dk46.