*****************************
Wabunifu kwenye Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya kati wameaswa kuzisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bunifu zao ili waweze kuzilinda kisheria na kupata manufaa kutokana na jitihada zao.
Afisa Mwandamizi Utumishi na Utawala kutoka Idara ya Miliki Ubunifu (BRELA), Bw. Raphael Mtalima ametoa rai hiyo tarehe 13 Juni, 2022 katika warsha ya kuwajengea uwezo watumishi na watafiti kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Neslon Mandela (NM-AIST), Jijini Arusha.
Bw. Mtalima amesema kuwa Wabunifu na Wavumbuzi wengi hawajui taratibu za kulinda kazi zao ili ziweze kuwanufaisha ingawa wamewekeza nguvu nyingi na rasilimali katika kufanya tafiti mbalimbali mpaka kufikia hatua waliopo.
Amebainisha kuwa Sheria ya kulinda vumbuzi na bunifu mbalimbali ipo na BRELA imekusudia kutoa elimu juu ya taratibu za kusajili katika vyuo vilivyopo Jijini Arusha kwa ajili ya kutoa elimu juu ya masuala ya kisayansi.
“Lengo kuu la warsha hii ni kuwajengea uwezo Wabunifu ili wajue umuhimu wa kuendelea na tafiti zao na kuzisajili BRELA ili waweze kunufaika hapo badaye,” amesema Bw. Mtalima.
Wakiwa Jijini Arusha, Maafisa wa BRELA pia watatoa elimu hiyo katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo Kikuu Cha Makumira.
Naye Mkuu wa Idara ya Utafiti na Ubunifu katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Bi. Edna Makule amesema Taasisi hiyo imefanya tafiti na bunifu mbalimbali zilizofikia hatua ya kulindwa, hivyo elimu hiyo ina manufaa kwao na watapiga hatua zaidi katika ulinzi wa bunifu zao.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa Warsha hiyo, mwanafunzi anayesoma Shahada ya Uzamivu (PhD) chuoni hapo, Bw. Isack Kandola amesema amejifunza mambo mengi kupitia BRELA na atatunza Bunifu zake ili zisiibiwe na watu wengine kutoka nje ya nchi na kusisitiza wabunifu kutunza mawazo yao kupitia Taasisi hiyo.