Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na jamii ya wawindaji ya Wahdazabe katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama mkoani Singida alipokwenda kutoa hatimiliki za kimila kwa wananchi wa jamii hiyo Juni 11, 2022. Wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida Sophia Kizigo akizungumza wakati wa zoezi la utoaji hatimiliki za kimila kwa jamii ya wawindaji ya Wahdazabe katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza Juni 11, 2022.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo wakiwapungia mkono wananchi wa jamii ya wawindaji ya Wahdazabe wakati wa zoezi la utoaji hatimiliki za kimila kwenye kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida Juni 11, 2022.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimpatia hatimiliki ya kimila Chifu wa jamii ya wawindaji ya wahadzabe Edward Mkumbo kwenye kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama mkoani Singida Juni 11, 2022. Wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo,
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa jamii ya wawindaji ya Wahdazabe kwenye kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza mara baada ya kuwakabidhi Hatimiliki za kimila Juni 11, 2022.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoka kwenye nyumba ya Chifu wa Jamii ya wawindaji ya Wahadzabe katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama mkoani Singida Juni 11, 2022. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha na Jamii ya wawindaji ya Wahadzabe katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama mkoani Singida mara baada ya kutembelea nyumba ya chifu wa jamii hiyo wakati wa ziara ya utoaji hatimiliki za kimila Juni 11, 2022.
Chifu wa jamii ya wawindaji ya wahadzabe Edward Mkumbo akiwa amesishikilia hatimiliki ya ardhi mara baadhi ya kukabidhiwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama mkoani Singida Juni 11, 2022. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
************************
Na Munir Shemweta, WANMM MKALAMMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameipongeza jamii ya wawindaji ya wahadzabe iliyopo wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa utayari iliyouonesha wa kutambua na kukubali kupimiwa maeneo yao na kupatiwa hatimiliki za kimila.
Jumla ya hatimiliki za kimila mia moja (100) zikiwemo 26 zinazomilikiwa kwa pamoja kati ya mke na mume zimetolewa kwa jamii ya wawindaji ya Wahadzabe ikiwa ni hatua kubwa kutokana na jamii hiyo kujishughulisha zaidi na uwindaji, utafutaji matunda, urinaji asali na uchimbaji mizizi.
Dkt Mabula alisema, hatua hiyo inaonesha nia na dhamira njema waliyonayo ya kutaka kuyalinda maeneo yao wenyewe na kwa kushirikiana na serikali.
‘’Hakika hizi ni salamu na ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa jamii ya wawindaji inaungana naye na mkoa tayari kwenda naye sambamba katika kuletea watu wote maendeleo’’ alisema Dkt Mabula.
Akizungumza na wananchi wa jamii ya wawindaji ya Wahadzabe katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama Juni 11, 2022 alisema, jamii hiyo ni miongoni mwa jamii ndogo nchini ambayo iko katika hali ya kupoteza ardhi wanayoimiliki kutokana na jamii nyingine kuingia na kufanya shughuli zisizoendana na tamaduni za jamii hiyo jambo alilolieleza linahatarisha ustawi na maisha na desturi za Wahadzabe.
‘’Katika miaka ya hivi karibuni jamii hii imekuwa ikikabiliwa na tishio la kutoweka na kupoteza uhalisia wa maisha yao baada ya jamii nyingine kuingia katika maeneo ya mapori ya asili yanayotumiwa na Wahadzabe kwa ajili ya kufanya shughuli za ufugaji, ukulima na hata upasuaji wa mbao jambo alilolieleza limekuwa tishio kwa kiasi kikubwa kwenye jamii hii’’ alisema Dkt Mabula
Alitolea mfano wamatishio kwa jamii hiyo kuwa ni pamoja na kupotea kwa makazi ya asili yanayojengwa kwa nyasi kavu chini ya matawi ya miti, wanyama kutoweka, mizizi na matunda kupotea kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli nyingine ambazo hazilindi uoto wa asiili wa mapori hayo.
Hata hivyo, alisema kuwa, kwa kutambua athari iliyopo mbele ya jamii hiyo ya wahadzabe, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitafuta njia bora ya kulinda jamii hiyo pamoja na jamii nyingine zinazofanana ili kuhakikisha inajenga jamii yenye usawa kwa watumiaji wote wa rasilimali za ardhi nchini.
Aidha, katika kuleta usawa Serikali imeendelea na program mbalimbali kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapimwa kwa lengo la kuruhusu usawa na ustawi siyo tu wa binadamu bali wa viumbe vyote vyote hai nchini.
‘’Ukiachilia mbali ukuzaji na uhifadhi wa tamaduni za jamii ya uwindaji kiloichonifurahisha zadi ni kuona jinsi jamii ilivyostaarabika kwa kuona na kuelewa umuhimu wa baba na mama kumiliki ardhi kwa pamoja , kwa hili niwapongeze’’ alisema Dkt Mabula.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo alisema, jamii ya Wahadzabe katika eneo hilo la kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya mgogoro wa mpaka unaosababisha maeneo wanayotegemea kwa shughuli zao kuharbiwa.
‘’Changamoto kubwa ya hapa, jamii ya Wahadzabe vyakula wanatoa porini, wanakula asali na nyama zakuwinda na misitu ikiharibiwa au maeneo wanayotegemea kupata vyakula yanapoharibiwa ni changamoto kubwa, hata hivyo niwapongeze kwa uvumilivu wao’’ alisema Kizigo.
Bosco Charles Samweli, Diwani wa Kata ya Mwengeza alimueleza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula kuwa, eneo hilo la jamii ya Wahadzabe kwa muda mrefu limekuwa na changamoto ya migogoro ya mpaka na wananchi wanaoishi wilaya za jirani za Karatu Arusha na Mbulu mkoa wa Manyara. Hata hivyo alisema kwa sasa changamoto zinaelekea kumalizika kutokana na juhudi kubwa za mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo.