Mbunge wa Afrika Mashariki kutoka Rwanda ,Balozi Fatuma Ndangiza akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha (Happy Lazaro)
…………………………………………..
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameliomba Bunge hilo kuandaa mswada wa kupitisha sheria ya kuwaenzi viongozi mbalimbali waliotangulia mbele za haki ili kuendelea kuyaenzi yale waliyoanzisha na kujenga utamaduni huo.
Wameyasema hayo leo juni 10 ,2022 bungeni hapo wakati wabunge hao wakiwapongeza na kuwaenzi aliyekuwa Spika wa bunge la Uganda Hayati Jacob Oulanyah na hayati Rais mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki kwa kudumisha demokrasia na utawala bora.
Akichangia hoja hiyo Mbunge wa Afrika Mashariki kutoka Rwanda,Balozi Fatuma Ndangiza amesema kwamba ipo haja kwa Bunge hilo kuandaa mswada wa kupitisha sheria ya kuwaenzi viongozi waliotangulia mbele za haki ili kuendelea kuwaenzi kwa mambo mbalimbali waliyoanzisha ambayo yanaleta maendeleo kwa nchi yetu na yanahitajika kuendelezwa .
Amesema kuwa, ukiangalia nchi ya Kenya imekuwa ikisifika kwa katiba bora,hapa utaona mchango mkubwa uliotolewa na hayati Mwai Kibaki kujenga Demokrasia wakati wa uongozi wake na hivyo hayo yote ni lazim yaenziwe na kuendelezwa na wakifanya hivyo ni sisi wenyewe.
Amesema kuwa,viongozi hao wanafaa kuigwa kwa mema yao yote na kuendelezwa na Bunge hilo kuendelea kuwaenzi na kukumbuka mchango wao kwa Taifa lao na mataifa ndani ya Jumuiya.
“Mwai Kibaki alianzisha Katiba na kutoa mchango mkubwa ili nchi iwe na katiba nzuri sasa hivi miongoni mwa katiba ya viwango ni ya Kenya hii inasaidia nchi kuwa na amani na hata Uhuru katika kutekeleza majukumu yake kutokana na msingi bora uliowekwa na viongozi husika” amesema Ndangiza.
Ameongeza kuwa, Bunge hilo linahitajika kuendelea kujenga Utamaduni huo endelevu wa kukumbuka viongozi wetu kwa wabunge kuleta muswada ili uingie kwenye sheria za Jumuiya hiyo ili iweze kuwa kitu endelevu.
“Hayati Spika Jacob alisaidia demokrasia ya nchi yake ,alitoa mchango kwa jamii kuwasaidia wenye maisha ya chini na yatima na kuendeleza demokrasia ambayo ikiigwa na vijana itawasaidia kwa kiwango kikubwa Sana.”amesema Balozi Fatuma.
Ameongeza kuwa, ni vizuri jamii zetu katika nchi za Jumuiya zijenge Utamaduni wa kuwaenzi viongozi waliotenda makubwa na kujenga misingi ya ukombozi demokrasia na utawala bora.