Na Lucas Raphael,Tabora
WALIMU, wazazi na walezi wanaowafanyia vitendo vya unyanyasaji kingono watoto wa kike au wa kiume wameonywa vikali na kutakiwa kuacha tabia hiyo mara moja kabla ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Onyo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batida Burian alipokuwa akiongea na mamia ya wakazi wa Vijiji vya Maguguni na Ugaka katika kata za Mtungulu na Ugaka wilayani Igunga.
Alisema vitendea hivyo vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku huku jamii ikikaa kimya badala ya kutoa taarifa ili wahusika wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Alibainisha kuwa vitendo vya namna hii huathiri watoto kisaikolojia na kuwaharibia ndoto zao kielimu, hivyo akaomba jamii kutoa taarifa wanapoona watoto wakifanyiwa vitendo vya namna hiyo.
‘Natoa onyo kwa walimu, wazazi na walezi wanaowafanyia vitendo vya unyanyasaji wa kingono watoto wa kike au kiume, waache mara moja, tutawasaka kokote walipo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria’, alisema Balozi Dkt Batilda.
Balozi Dkt Batilda alifafanua kuwa dhamira ya serikali ni kuona watoto wote wanapata haki zao za msingi ikiwemo kutunzwa, kupendwa na kupewa elimu na sio kunyanyaswa kingono au kufanyiwa vitendo visivyofaa.
Aidha aliongeza kuwa ataunda timu maalumu itakayopita katika shule zote, mwalimu au mzazi yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo atakamatwa na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.
Alitoa mfano wa watoto 6,000 waliobainika kuacha shule kwa sababu mbalimbali Mkoani hapa ambapo waliwasaka na hadi sasa 3,000 wamepatikana na kurudishwa shuleni na baadhi ya wazazi waliohusika wamekamatwa na kuswekwa ndani.
Balozi Dkt Batilda alisisitiza kuwa anataka watoto wote wasome shule na hata wale wasio na wazazi au walezi ni lazima wasome hivyo akaomba wenye taarifa za watoto wasio na wazazi au ndugu wa kuwasomesha kutoa taarifa ili waangalie namna ya kuwasaidia.
Akiongea katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watafanyia kazi maelekezo hayo ili kuhakikisha vitendo hivyo vnakomeshwa miongoni mwa jamii.
Katika kuonesha kwamba vitendo hivyo havikubaliki na Viongozi wa wilaya na Mkoa wako makini hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Paul Chacha aliagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani Mwalimu wa Nidhamu wa shule sekondari Igwisi kwa tuhuma za kubaka na kumsimamisha Mwalimu Mkuu kwa kutochukua hatua ya kukomesha tbi hiyo licha ya kupewaa taarifa.