Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian akiongea na wananchi Wilayani Kaliua Mkoani Tabora hivi karibuni katika hafla ya uzinduzi wa miradi wa miradi wa maji iliyotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilayani humo.
……………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Salha Burian ameagiza Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri na Maofisa Nyuki wote Mkoani hapa kuhamasisha miradi ya ufugaji nyuki katika wilaya zao ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao hilo.
Ametoa agizo hilo jana katika kikao cha wadau wa ufugaji nyuki na kilimo kilichofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini hapa na kuhudhuriwa na Wakuu wa wilaya zote, Wakurugenzi, Wataalamu na Maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na TAWA.
Alisema kuwa asali ni miongoni mwa mazao yanayoziingizia mapato mengi halmashauri na taifa kwa ujumla hivyo linapaswa kupewa kipaumbele na kuhamasishwa ili liwe zao kubwa la kiuchumi katika Mkoa huo.
Alisisitiza kuwa asali inayozalishwa Tabora ni ya asili na ina ubora wenye virutubisho vyote ndio maana inapendwa na watu wengi ndani na nje ya nchi, hivyo mkakati wa kwanza ni kuhamasisha uzalishaji na kubuni nembo maalumu itakayotambulisha asali inayozalishwa katika Mkoa huo.
‘Asali ina manufaa makubwa sana kwa jamii, kwanza ni tiba, kiburudisho na biashara nzuri, hivyo mbali na mazao mengine ya chakula na biashara tunayolima, zao hili tukilipa kipaumbele litachochea kasi ya uchumi wa wakulima, mkoa na taifa kwa ujumla’, alisema.balozi Dkt Batilda
Ili kuifanya shughuli ya ufugaji nyuki kuwa endelevu Dkt Batilda aliwataka Wataalamu wa Kilimo na wakulima kwa ujumla kuacha kutumia madawa ya kilimo yenye madhara makubwa kwa nyuki, alitoa mfano wa dawa ya Salfa kuwa inafukuza nyuki kutokana na harufu yake.
Alitoa wito kwa wafuga nyuki wote kutumia mizinga ya kisasa ili kurahisisha zoezi la uvunaji asali na mazao mengine ya nyuki wakati wa mavuno, aidha aliagiza halmashauri kutenga bajeti ili kusaidia wajasiriamali wanaozalisha asali.
Ili kuleta tija katika mkakati huo aliwataka Maofisa Nyuki na Wataalamu kutoka Chuo cha Nyuki Tabora kutoa mapendekezo ili Mkoa mzima uwe na siku maalumu (Kalenda) ya utundikaji mizinga na uvunaji asali ili kuboresha zao hilo.
‘Ili kuongeza uzalishaji wa asali na mazao mengine ya nyuki, nataka kila mfugaji aongeze idadi ya mizinga na bei ipunguzwe ili kila mtu amudu kuinunua, nataka tufikishe mizinga 200,000 ya kisasa katika Mkoa mzima’, alisema. Balozi Dkt Batilda
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tabora Dkt Yahaya Nawanda aliunga mkono maono hayo na kumhakikishia RC kuwa asali yote inayozalishaji na vikundi vya wajasiriamali itaongezewa thamani ili kuvutia watu wengi zaidi.
Aidha alibainisha kuwa wanaangalia uwekezekano wa kutenga eneo ambalo litakuwa ‘Kituo maalumu cha kuuzia asali na mazao mengine ya nyuki’ ili kurahisisha upatikanaji wa mazao hayo kwa wageni wanaotembelea Mkoa huo.