*************************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
ZAO la kibiashara la Ufuta ,limeanza kuonyesha tija katika Mkoa wa Pwani, ambapo hadi sasa mauzo yamefikia kilo milioni 6,500,505 zenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni 18.
Akikabidhi pikipiki Tisa kwa maafisa Ushirika wa Halmashauri za mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alifafanua, mauzo hayo ni minada miwili tu kwa msimu wa mwaka huu 2022/2023.
Alisema ,hili Ni ongezeko na neema kwa wakulima wa Ufuta tofauti na msimu uliopita wa mwaka 2021 ambapo Tani 13,000 ziliuzwa na kupatikana zaidi ya sh.Bilioni 28.
Kunenge alieleza , maafisa wa Ushirika ,maafisa ugani watapimwa kwa usimamizi wao kwa kuangalia hali ilivyo Sasa ,matarajio na baada ya kupatiwa usafiri kuwe na matokeo chanya.
“Mazao yanayopatikana katika mkoa wetu yapo mazao ya chakula ,ya baharini ikiwemo Mwani na mazao ya biashara kama korosho,miwa,ufuta na Mchikichi”
“Tumepata tija katika mazao haya ila bado haitoshelezi , matarajio ni makubwa muendelee kujipanga, Uwezo wenu mkaonyeshe katika utendaji halisi na kuangalia matarajio makubwa ili kuhakikisha dhamira ya Rais ya kutumia fedha kidogo kuwapatia vitendea kazi inaleta mafanikio”alifafanua Kunenge.
Aidha Kunenge alibainisha kwamba, wameangalia mnyororo wa thamani wa kila kilimo na kubaini baadhi ya changamoto kwenye usimamizi wa maafisa Ushirika ili kutembelea vyama vya ushirika .
Awali Mrajisi Msaidizi Mkoani Pwani ,Angela Nalimi alisema wanaendelea na minada ya ufuta kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na wameshauza Tani 6,500 sawa na kilo milioni 6.5.
Hata hivyo ,alitaja changamoto za usimamizi wa shughuli za ushirika kutokana na uhaba wa vitendea kazi ikiwemo usafiri na kumshukuru Rais kwa kutoa usafiri kupitia Wizara ya Kilimo pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
Ofisa ushirika Halmashauri ya Chalinze, Raphael Kajale alisema , Chalinze ina kata 15 nyingine zipo pembezoni hivyo Basi usafiri huo umekuja wakati muafaka , itasaidia kutekeleza na kusimamia majukumu yao ya kazi .
Mkoa wa Pwani una vyama vya ushirika 166 ambavyo kati yake AMCOS ni 105 ,Sacco’s 37 vya aina nyingine 24 na vyama kumi vipo kwenye matazamio.