Mkuu wa Ofisi ya WFP Kibondo akielezea namna shirika hili lilivyoinua wakulima wilayani humo kupitia Mradi wa KJP.
Kaimu Mkuu WFP Kasulu, Michael Bisama akielezea namna shirika hili lilivyoinua wakulima wilayani hapo kupitia Mradi wa KJP.
Mratibu wa KJP Halamshauri ya Kasulu Vijijini, Masatu Pima akionesha maharagwe ambayo yanasafishwa baada ya kufikishwa katika Chama cha Ushirika Kurugongo.
Bizimana Josephat na Msa Boy wakipukuchua mahindi kwa kutumia mashine ya kisasa ambapo inaweza kupukuchua gunia 50 kwa muda mchache.
Mkulima Juma Sharifu wa kijiji cha Kurugongo akimuonesha Ofisa Mradi wa KJP Halmashauri ya Kasulu Mji maharagwe ambayo wamevuna na kuyafikisha kwenye Chama cha Ushirika.
Wakulima wa mahindi kijiji cha Nyumbigwa wakivuna mahindi kwa njia bora katika moja ya shamba la mkulima mwenzao.
Beatha Rafael akieleza namba ambavyo amenufaika kwa ujio wa WFP na Mradi wa KJP na manufaa ambayo ameyapata.
Mkulima Mzee Sospeter Mkula akionesha waandishi mahindi ambayo ameyahifadhi kwa njia yenye ubora.
……………………………………..
Na Selemani Msuya, Kigoma
SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kupitia Mradi wa Kigoma Joint Program (KJP), wamewezasha wakulima 24,000 wa wilaya tatu za Kasulu, Kibondo na Kakonko mkoani Kigoma kuongeza uzalishaji wa mazao ya maharagwe, mahindi na muhogo.
Mradi KJP katika eneo la kilimo unatekelezwa na WFP, Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC), Shirika la Uendelezaji wa Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) katika halmashauri hizo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Ofisi ya WFP Kibondo, Saidi Johari wakati akizungumza na waandishi wa habari waliopo kwenye ziara ya kuangalia namna KJP upande wa kilimo ilivyofanikiwa kuinua wakulima mkoani humo.
Johari alisema katika kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji WFP kwa kushirikiana na halmashauri walianza kutambua vikundi 1,255 na kutoa mafunzo kwa wakulima namna ya uhifadhi na kuzuia upotevu wa mazao kwa wakulima 24,316 kuanzia mwaka 2018.
Alisema WFP imetumia Sh.milioni 596 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi ambazo zimegawanyika katika maeneo manne muhimu.
“Tumekarabati maghala matano katika Wilaya ya Kasulu na Kibondo kwa Sh.milioni 137, kujenga miundombinu ya kukaushia mazao Sh.milioni 237, kununua maturubai, vifaa vya kupimia unyevu, mbao za kuwekea mazao kwa Sh.137 na mashine 27 za kupukuchua mazao Sh.milioni 84,” alisema.
Mkuu huyo wa ofisi alisema baada ya uwekezaji huo wakulima hasa wa mahindi na maharage waliweza kuongeza uzalishaji kwa kupunguza upotevu wa mazao kutoka asilimia 28 hadi kufikia asilimia 12, hivyo kuwapatia faida kubwa zaidi.
“Mradi wa KJP katika eneo la kilimo kila mdau anashiriki eneo lake, mfano FAO wanaangalia mchakato wa kilimo bora, WFP tunaangalia upotevu wa mazao, ITC wanafanya mambo ya masoko na UNCDF wanaangalia mambo ya fedha,” alisema.
Mkuu huyo wa ofisi alisema mradi huo umewezesha wakulima kuiuzia WFP tani 366 za maharagwe bora katika msimu wa mwaka 2019/2020 na kuwaingizia Sh.milioni 751 na mwaka 2020/2021 waliiuzia WFP tani 1,315 na kuingiza Sh.bilioni 2.5.
Johari alisema katika utekelezaji wa mradi pia wameshirikisha wadau wengine ambapo wametumia Sh.bilioni 4.5 na kwamba hadi sasa mradi huo umegharimu Sh.bilioni 5.
“Kimsingi mradi huu katika misimu miwili umeweza kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh.bilioni 3, kupitia maharage waliyouza kwa WFP hivyo tunadiriki kusema una manufaa makubwa ni matarajio yetu kwamba pamoja na kufikia mwisho Juni 30 mwaka huu utaendelezwa,” alisema.
Akizungumzia na waandishi wa habari Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Rashidi Mchatta alisema WFP ni moja ya mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa (UN) ambayo yamefanikisha mradi wa KJP katika eneo la kilimo, hali ambayo inachangia ongezeko la mapato kwa wakulima na mkoa kwa ujumla.
“Mfano Wilaya ya Kasulu wamekarabati maghala matatu kwenye vijiji vya Kigadiye, Kurugongo na Nyakitonto. Pia WFP wameanzasha vyama vya ushirika na kuviunganisha na masoko, hivyo mkulima ana uhakika na soko,” alisema.
Katibu Tawala huyo alisema pia WFP wametoa elimu na kuwawezesha maofisa ugani kuwa karibu na wakulima, hivyo wamechangia ongezeko la mazao.
Mchatta alisema Serikali ya mkoa itahakikisha mafanikio hayo yanaendelezwa na kusambazwa kwa wakulima wote mkoani hapo.
Naye Mshauri wa Kilimo Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma, Joseph Rubuye alisema WFP wamechangia kuongeza usalama na mnyororo wa thamani ya chakula, hivyo kunufaisha mkulima.
“Hawa WFP wamefanya mapinduzi katika kilimo kwenye wilaya hizo tatu, hivyo jukumu letu ni kuhakikisha mafanikio haya yanafikia kila ambapo kuna mkulima,” alisema.
Rubuye alisema Kigoma kuna zaidi ya wakulima laki tatu, lakini wakulima 24,316 waliofikiwa watakuwa mabalozi wazuri kwa wenzao.