***********************
Na Mwandishi Wetu, Bukoba
WAENDESHA pikipiki maarufu kama bodaboda mkoani Kagera wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupunguza gharama za mafuta, huku wakiomba kazi yao irasimishwe.
Hatua ya kupunguza bei ya mafuta ilitokana na mtazamo chanya wa serikali wa kubana matumizi na kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100, jambo ambalo limesaidia kushuka kwa bei hapa nchini na kupunguza makali ya maisha.
Pongezi za bodaboda hao zimewasilishwa na Umoja wa Bodaboda wilayani Bukoba (UBOBU) ikiwa ni siku moja kabla ya Rais Samia kufika mkoani Kagera kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.
Mwenyekiti wa UBOBU, Mahamud Sued alisema ushushaji wa bei ya mafuta utalisaidia kundi hilo kuweza kumudu gharama za maisha na kuepuka kujiingiza kwenye vitendo viovu.
“Ili kutambua ukubwa wa kundi hili kwa upande wa Manispaa ya Bukoba pekee kuna bodaboda 8,600 ndio maana tunaomba aendelee kutupunguzia bei ya mafuta.
Ruzuku imetolewa kwa wakati muafaka na kutupa ahueni sisi ambao riziki zetu zinategemea sana bei ya mafuta.”
Alisema kabla ya kutolewa kwa ruzuku hiyo, kwa Bukoba mafuta yalikuwa yanauzwa shilingi 3,460 kwa lita na sasa yanauzwa shilingi 3,200 kwa lita kukiwa na punguzo ya shilingi 260 kwa lita.
“Pia tunamuomba Rais Samia kurasimisha biashara ya bodaboda na kulitambua kama kundi maalum lenye uhitaji wa kuwekewa mazingira mazuri ya kibiashara kama inavyofanyika kwa wamachinga.
Kundi hili tupo watu wa kila aina, kuanzia waliomaliza darasa la saba au chini zaidi mpaka waliomaliza vyuo vikuu lakini wakakosa ajira. Wote tumejiingiza humu na kujiajiri kutafuta kipato ili kulea familia na wategemezi wetu kwa kufanya kazi halali ya uendeshaji wa bodaboda,” alisema Sued.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Steven Byabato alisema katika suala la kutoa ruzuku hiyo, Rais Samia ameupiga mwingi tena wa kimataifa kwa sababu mafuta hayajashuka bei bali Rais Samia ameshusha bei ya mafuta kwa kuweka hiyo fedha ya ruzuku.
Alisema kinachotakiwa ni kumuombea ili Rais Samia aweze kupambana kutafuta namna ya kushusha zaidi bei hiyo kwa kutafuta fedha nyingine zitakazosaidia punguza gharama kwa wananchi.
“Kwa sababu isingeweka hiyo ruzuku sasa hivi Bukoba tungekuwa tunanunua mafuta 3,700 au 3,800 pengine hata na zaidi.
Na bei hiyo inaendelea kupanda duniani kwa sababu upatikanaji wa bidhaa hiyo ni mdogo kuliko uhitaji wake ambao ni mkubwa,” alisema Byabato.
Byabato alisema kwa Tanzania mafuta hayashuka bali kutokana na huruma ya Rais inayotokana na umama ameamua kuweka fedha hizo ili kushusha bei kwa lengo la kupunguza ukali wa maisha.
“Katika kitu ambacho Rais Samia ametusaidia ni kuweka shilingi bilioni 100, na ninawaahidi huko tunakoelekea ni kuzuri zaidi,” alisisitiza.