Na Mwamvua Mwinyi, Kibiti
MKUU wa Wilaya ya Kibiti kanal Ahmed Abbas ameeleza ,kumekuwepo na usimamizi wa miradi usioridhisha na mapungufu na upotevu mkubwa wa Raslimali fedha na vifaa kwenye baadhi ya miradi wilayani humo, ambapo baadhi ya watu wachache wanajinufaisha kinyume na Utaratibu.
Aidha , ameziagiza Taasisi za serikali zinazosimamia na kutekeleza miradi ikiwemo RUWASA , TANESCO na TARURA, kufuata taratibu za kuweka wakandarasi ili kuepuka hujuma katika miradi ambayo Serikali imekuwa ikipata hasara.
Akitoa maagizo hayo wakati akifungua kikao cha Baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka ,alisema Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Serikali ya awamu ya sita analenga kutatua changamoto za miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara,maji na umeme na matarajio ni kuona miradi hiyo inanufaisha jamii.
“Usimamizi wa miradi usioridhisha yapo mapungufu, mkienda kwenye miradi mnayabaini mlioenda, wakati ndani ya miradi kuna kamati zinazohusika kusimamia kupitia mapungufu hayo kuna upotevu mkubwa wa Raslimali fedha na vifaa”
Kanal Ahmed alitoa Rai kamati hizo zitekeleze wajibu wake na mtu atakaebainika amekiuka taratibu achukuliwe hatua za kinidhamu na kurejesha alichokipoteza .
“Watu hawa wamekuwa wakipelekwa mahakamani, nasisitiza arejeshe kwanza alichopoteza kwani akifungwa haitoshi”alifafanua Ahmed.
Pia alisisitiza Halmashauri kuhakikisha inatengeneza mifumo mizuri ya makusanyo na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha.
Pamoja na hayo, kanal Ahmed ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Usalama wilaya alisema, kwa kutofuata maagizo na maelekezo ya Serikali yanayotolewa unasababisha kutoa mianya yakuonyesha wilaya au Halmashauri haifanyi vizuri kutokana na wananchi kuendelea kutoa malalamiko.
“Nikipokea malalamiko kutokana na utoaji vibali vya ufuta wakati Serikali suala hili ilishatoa maelekezo vibali visiwepo na ufuta uuzwe kupitia stakabadhi ghalani .”
Kufuatia suala hilo ,kanal Ahmed ameunda kamati ya uchunguzi ambapo kamati hiyo tayari ipo kazini ikikamilisha kazi itatoa ripoti ya uchunguzi.
Nae mbunge wa jimbo la Kibiti ,Twaha Mpembenwe alisema ,hatokubali kuona wakandarasi wanakwamisha miradi ya barabara ama maji kwani kwa kufanya hayo kunasababisha miradi kusuasua.
Aliwataka watendaji wa Halmashauri ,madiwani Kujenga tabia ya kuwa na nguvu ya kufanya Maamuzi wanapobaini wakandarasi wazembe kwa maslahi ya wananchi.
Mpembenwe alimshukuru ,Rais Samia kwa kupeleka fedha za miradi ya maji kiasi cha sh.bilioni 3.9, na kwa kuunga mkono jitihada hizo za Serikali amepata wafadhili wanaondelea kuchimba visima vya maji 400 katika jimbo hilo.
Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji na barabara , Diwani wa kata ya Mwambao Khatibu Chaurembo , Diwani wa Kibiti Hamidu Ungando , na Diwani wa kata ya Dimani Yusuph Mbinda walibainisha ,mwaka wa fedha 2021-2022 unakamilika na baadhi ya miradi haijakamilika licha ya fedha za miradi hiyo zipo.
Alitoa ufafanuzi ,Meneja wa RUWASA Kibiti, Pascal Kibang’ule alisema , wanatekeleza miradi sita kwa gharama ya Bilioni 3.9 kupitia fedha za mwaka wa fedha unaomalizika Julai mwaka huu.
Alisema kati ya miradi hiyo upo mradi huko Mahege unaotekelezwa kwa fedha za Uviko19 ambao umefikia asilimia 65 na yote inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Kibang’ule alieleza kwamba, miradi miwili imeingia kwenye changamoto ya kuchelewa kutokana na tatizo la mvua za mwezi February hadi April na sasa wakandarasi wanaendelea na kazi.