Meneja wa mradi wa Uhakika wa Maji Bi Pendo Hyera akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wakulima na wafugaji wa vijiji vya Chanzulu na Bwade ulioandaliwa na Mashahidi wa Maji
Mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Kilosa Mkunwa Suhani akitoa mtazamo wake juu ya namna wanaweza kutatua changamoto zilizopo baina yao kwenye mkutano uliowakutanisha wakulima na wafugaji wa vijiji vya Chanzulu na Bwade ulioandaliwa na Mashahidi wa Maji
Picha ya pamoja baada ya mkutano uliowakutanisha wakulima na wafugaji wa vijiji vya Chanzulu na Bwade ulioandaliwa na Mashahidi wa Maji
……………………………………………….
Na Farida Juma,Kilosa
Shirika la Shahidi wa Maji kupitia mradi wake wa Uhakika wa Maji umefanikiwa kumaliza mgogoro wa rasilimali maji kati ya wakulima na wafugaji wa vijiji vya Chanzulu na Mbwade Wilayani Kilosa uliodumu kwa miaka mingi.
Mgogoro huo wa kugombania maji ya mto Ilonga kwa ajili ya shughuli zao za Kilimo na Ufugaji umemalizika kwa kuwakutanisha Watu hao wa jamii mbili na kukubaliana namna bora ya kila upande utakavyonufaika.
Wakizungumza kwenye kikao kilichoandaliwa na Mashahidi wa Maji kwa kuwakutanisha wakulima na wafungaji na hudhuliwa na viongozi wa vijiji pamoja na Mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Kilosa bwana Mkunwa Suhani, walisema lengo la kikao hicho ni kutatua sintofahamu iliyopo kati yao na kuweka usawa wa matumizi sahihi ya maji katika Mto Ilonga kwa jamii zote mbili.
Walisema pamoja na mabadiliko ya tabianchi kuchangia kwa kiasi kikubwa upungufu wa maji katika Mto Ilonga pia shughuli za kibinadamu zinazofanywa kandokando ya mto huo zinapelekea maji kuacha njia na kuufanya mto kukosa uhai na kubadili uelekeo wake.
Kutokana na hali hiyo wakulima na wafugaji hao waliomba serikali pamoja na wadau wa mazingira kuweza kuwapa elimu ya namna gani wanaweza kufanya shughuli zao bila ya kuathiri vyanzo vya maji.
“Tunaiomba serikali ikiwezekana watuletee miti ya matunda tuweze kupanda pembezoni mwa mto pia watupe elimu ni mazao gani tunaweza kulima bila ya kuharibu mazingira.”Alisema Bi Felista Mbago.
Akichangia katika kikao hicho Bwana Julius Ndaiga ambaye ni mkulima katika skimu ya umwagiliaji ya Chanzulu alisema kuna haja ya kuweka mkakati wa kufanya usafi katika mto huo ili jamii zote ziweze kupata maji bila ya malalamiko yoyote kwani maji mengi yamekuwa yakienda katika skimu ya Ilonga kutokana na mto huo kutofanyiwa usafi na kusababisha kujaa kwa mchanga.
Pia alitoa wito kwa wafugaji kushiriki zoezi la kufanya usafi katika mto kwani wamekuwa wazito katika zoezi hilo hali inayowasababisha kukosa maji na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji kwa ajili ya mifugo yao.
Nae Bwana Sungai Zakayo ambaye ni Mfugaji aliomba kamati ya mazingira kwa kushirikiana na Mashahidi wa Maji kuchua hatua kwa mtu yeyeote atakaye bainika kuharibu chanzo cha maji ili iwe funzo kwa wengine na kutunza vyanzo hivyo.
“Vyanzo vya maji vikiharibiwa tunaoteseka zaidi ni sisi wafugaji kwani tupo mwisho katika kupata maji na wakati mwingine hata hatuwekwi kwenye hesabu ya kupata maji.” alisema Bwana Zakayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Kilosa Mkunwa Suhani alisema pamoja na mambo mengine kikao hicho kimeleta mwanga wa mafanikio katika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani humo.
Aidha alilishukuru shirika la Shahidi ya Maji kuweza kuwakutanisha wakulima na wafugaji ambapo alisifu na kusema ni hatua kubwa sana ambayao haijawahi kutokea huku akiahidi kufanyia kazi yale yote waliyokubaliana katika kikao hicho.
Nae meneja wa mradi wa Uhakika wa Maji Bi Pendo Hyera alitoa wito kwa wakulima na wafugaji kuwatumia Mashahidi wa Maji katika kupaza sauti zao ili changamoto zinazowakabili hasa katika matumizi ya rasilimali maji kwa jamii hizo mbili kutatuliwa kwa njia ya amani.
Wakizungumza katika mkutano huo wawakilishi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa walisema watazifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa katika ofisi hiyo huku wakisifu kazi kubwa iliyofanywa na Mashahidi wa Maji ya kuwakutanisha wakulima na wafugaji katika kuwajengea uwelewa wa matumizi mazuri ya rasilimaji.
Shahidi wa Maji ni Shirika lisilo la kiserikali linalo tekeleza mradi wa Uhakika wa Maji katika Wilaya mbili za Kilosa na Kilombero ukiwa na lengo la kutambua uwajibikaji wa viongozi wa serikali katika kutatua changamoto za upatikanaji wa maji na usawa wa maji kwa shughuli za Kilimo,Mifigo na Uvuvi.