Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)Mhandisi Patrick Kibasa kushoto, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji Pambazuko-Mlele unaotekelezwa kwa fedha mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uvico-19 kwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,wa pili kulia Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza jana wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji Pamnazuko-Mlete katika manispaa ya Songea unaotekelezwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Songea(Souwasa) kwa gharama ya Sh.milioni 546,104,330.30,kulia Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Oddo Mwisho.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiangalia sehemu ya kisima cha maji kitakachotumika kwenye mradi wa maji Pambazuko-Mlete unaotekelezwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 546,katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Souwasa Mhandisi Patrick Kibasa na kushoto Meneja Ufundi wa Mamlaka hiyo Mhandaisi Jafari Yahaya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)Mhandisi Patrick Kibasa wa pili kushoto,akimuonesha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wa kwanza kulia kisima cha maji kitakachotumika kwenye mradi mkubwa wa maji wa Pambazuko-Mlete,wa pili kulia Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema na kushoto Meneja Ufundi wa Souwasa Mhandisi Jafari Yahaya.
Baadhi ya wataalam kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa) na wataalam wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Ruvuma wakiangalia tenki la kuhifadhia maji linaloendelea kujengwa kupitia mradi wa maji Pambazuko-Mlete utakaowanufaisha xzaidi ya wakazi 3,9990.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kushoto,akimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa huo Oddo Mwisho kabla ya kutembelea na kukagua mradi wa maji Pambazuko-Mlete unaotekelezwa kwa fedha za Mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uvico-19 katika Manispaa ya Songea wilayani Songea.
…………………………………….
Na Muhidin Amri,
Songea
MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji utakaowanufaisha zaidi ya wakazi 3,990 wa mtaa wa Pambazuko na Mlete katika Manispaa.
Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 546,104,822.18 fedha zilizotolewa na Serikali kupitia wizara ya maji chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.
Hayo yamesemwa jana Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea (Souwasa)Patrick Kibasa wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Alisema,mradi huo unajengwa na kampuni ya Jambela Limited na ulianza kutekelezwa tarehe 28 Disemba mwaka jana na unatarajiwa kukamilika tarehe 28 Juni 2022 na muda wa utekelezaji wake ni miezi sita na mkandarasi ameshalipwa jumla ya Sh.milioni 454,526,655.72 sawa na asilimia 83 ya fedha zote.
Alisema,mradi utakapokamilika pia unatarajia kuwanufaisha wanachuo wa chuo cha Uhasibu Arusha Tawi la Songea ambapo alitaja vyanzo vya maji vya mradi ni visima viwili vyenye uwezo wa kuzalisha lita 518,400 kwa siku na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 75.
Kibasa alisema,kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa nyumba mbili kwa ajili ya mashine za kusukuma maji(Pump House)kufunga pampu mbili katika vituo vya kusukuma maji,kufunga mfumo wa umeme,kujenga tenki moja la juu la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 150,000.
Kibasa alitaja kazi nyingine ni ujenzi wa uzio katika nyumba za pampu,kujenga uzio kuzunguka tenki,kuchimba mtaro na kulaza bomba za kusafirishia maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwenye tanki umbali wa km 3.5, kuchimba mtaro na kulaza bomba,ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji na mfumo wa kutibu maji.
Kwa mujibu wa Kibasa,hadi sasa kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba za pampu,ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji ambalo lipo kwenye hatua ya kupiga lipu,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji,kuchimba mtaro na kulaza bomba,kujenga uzio kwenye tenki na uzio katika nyumba za pampu ambapo mfumo wa umeme upo kwenye hatua ya kufunga waya kwenye nguzo.
Alisema,Souwasa inajenga mradi huo kwa kutumia wataalam wake wa ndani ili kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa ubora,usalama na kwa muda uliopangwa na Wizara ya maji imeshatoa fedha zote ili malipo ya mkandarasi yasichelewe.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,ameitaka Mamlaka hiyo kukamilisha mradi huo mapema ili wananchi waliolengwa kunufaika waweze kupata huduma ya maji haraka.
Pia alisema,mradi huo ni muhimu kwa kuwa katika eneo hilo linatarajiwa kujengwa chuo cha Uhasibu Arusha tawi la Songea, ambacho kitachukua watu wengi watakaohitaji huduma ya maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Generali Ibuge ametoa wiki moja kwa Shirika la Umeme(Tanzania)mkoa wa Ruvuma,inakamilisha kazi ya kuunganisha umeme ili utakaosaidia kuendesha mitambo ya mradi huo wa maji.