Mjumbe wa kamati iliyoandaa ripoti ya ukusanyaji maoni ya wananchi wilayani Ngorongoro mkoani Arusha , Edward Maura akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mapendekezo waliyoyakabidhi serikalini.(Happy Lazaro)
……………………………………………..
Happy Lazaro, Arusha
Arusha. Ripoti ya Kamati maalum ya viongozi na wataalamu juu ya mgogoro wa Ardhi ya Tarafa ya Ngorongoro, Sale na Loliondo iliyowasilishwa hivi karibuni kwa waziri mkuu, leo ripoti hiyo imewasilishwa kwa wananchi.
Ripoti ya mapendekezo hayo ni juu ya maoni ya wakaazi wa wilaya ya Ngorongoro, mambo wanayoyataka katika zoezi la kuhamishwa wananchi katika maeneo yao, ambayo wamedai kuwa, wanaofaa kuhamishwa ni wale waliokuja hivi karibuni na kujenga majumba makubwa sambamba na wale wanaotaka kuhama kwa hiari yao.
Maoni hayo yaliwasilishwa mjini Dodoma hivi karibuni kwa Waziri Mkuu na wawakilishi wa wakazi wa wilaya ya Ngorongoro wakiwemo Mbunge wa Ngorongoro Mhe. Emmanuel Shangai, Malaigwanani, Madiwani, wenyeviti wa vijiji, wawakilishi wa wanawake na vijana.
Akizungumza jijini Arusha, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Metui ole Shaudo amesema mchakato huo wa mapendekezo ya wananchi umedumu kwa muda wa miezi mitatu ili kuwafikia wananchi katika kwa wingi na waweze kutoa mapendekezo yao ambayo yote yameandikwa katika ripoti hiyo kwa ufupi.
“Tunatumaini mapendekezo haya serikali itatoa matokeo chanya kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa Ngorongoro na utaleta suluhu katika utatuzi wa migogoro ya ardhi katika eneo lenye kilometa za mraba 1500 bila kuathiri pande zote mbili,”amesema Mwenyekiti huyo.
Metui amesema hatua hiyo ilifuata baada ya mchakato wa kuwashirikisha wananchi na makundi mbalimbali katika jamii kuwa hafifu katika kutatua mgogoro huo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nainoka noka, Edward Maura amesema wanaishukuru serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu kwa kutoa fursa kwa wananchi wa wilaya ya Ngorongoro kuunda kamati na kuandika mapendekezo ya jamii juu ya mwenendo wa changamoto zilizopo wilayani hapo.
” kupitia kamati iliyokuwa na wajumbe wa pande zote katika jamii tumeikamilisha hiyo kazi kutokana na ushirikiano baina ya wananchi na wanakamati hali iliyoleta tija katika kuandika taarifa hiyo tuliyoiwasilisha serikalini,”amesema Diwani huyo.
Pia amesema wanamshukuru waziri mkuu kwa kupokea taarifa hiyo na kuwaahidi serikali kupitia Mbunge wa Ngorongoro kurudi kwa ajili ya majadiliano hivyo wanategemea taarifa hiyo kutoa mateokeo chanya.
“Kubwa sisi tuko tiyari kushirikiana na serikali katika kuitunza Ngorongoro yetu na katika mapendekezo hayo tumeandika jinsi ya kufanikisha Hilo bila kuathiri upande wowote Kati yetu na serikali kikubwa ni hifadhi yetu ibaki salama hadi miaka 1000 ijayo”
Awali Mei 25 mwaka huu waziri Kassim Majaliwa alipokea mapendekezo kutoka kwa wananchi wa Tarafa za Loliondo, Ngorongoro na Sale kuhusu namna bora ya kulinda uhifadhi wa maeneo hayo.