Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Lindi Dkt Dora Haule akizungumza na wataalam na wadau wa sekta ya misitu kutoka mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma kwenye mkutano wa kutafuta na kuboresha sekta ya misitu na nyuki katika mikoa hiyo,
Kamanda wa wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)kanda ya kusini Kamishina msaidizi Manyise Mpokigwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa sekta ya misitu na nyuki kwa washiriki wa mkutano wa wataalam wa sekta ya misitu kanda ya kusini,
Afisa Misitu Daraja la 1 wa wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)Kanda ya kusini Rweyemamu Kamugisha akizungumza katika mkutano wa wataalam wa misitu uliofanyika mjini Lindi.
Afisa Misitu Mkuu kutoka wizara ya Maliasili na Utalii James Nshare akizungumza katika mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)kanda ya kusini na wadau na wataalam wa sekta ya misitu kutoka mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma.
Afisa Maliasili wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Ombeni Hingi akizungumza wakati wa mkutano wa wataalam wa misitu wa mikoa ya Kusini.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga(hayupo pichani)kwenye mkutano wa wataalam wa sekta ya misitu.
wadau wa sekta ya misitu kanda ya kusini wakifuatilia mada mbalimbali katika mkutano wa wataalam wa misitu uliofanyika mjini Lindi.
Na Muhidin Amri,Lindi
…………………………………………………..
MKUU wa mkoa wa Lindi Zainab Teleck,amewataka wadau wa misitu kanda ya kusini kuunganisha nguvu zao ili kukabiliana na tatizo kubwa la uharibifu wa misitu, kulinda uoto wa asili ili kuwa na misitu endelevu kwa ajili ya maendeleo ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Teleck ametoa kauli hiyo jana,katika Hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wataalam wa misitu Kanda ya kusini uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa mjini Lindi.
Taleck alisema, uharibifu wa misitu usipodhibitiwa utasababisha gharama kubwa ya kurejesha uoto wa asili ulioanza kupotea na hata kusababisha kizazi kijacho kushindwa kupata matunda ya misitu iliyopo hapa nchini kutokana na tamaa ya baadhi ya watu wachache kutaka kujinufaisha wao binafsi.
Alisema,pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS) kanda ya kusini na wadau mbalimbali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira,lakini bado kuna kiwango kikubwa cha uhabifu wa mazingira ikiwamo tatizo la ukataji miti ovyo na uchomaji moto misitu hasa ya asili jambo linalotishia kwa kiwango kikubwa upotevu wa misitu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa ni kwamba Mkoa wa Lindi na Mikoa mingine ya Kanda ya Kusini ina Utajiri Mkubwa wa Rasilimali Misitu, hata hivyo pamoja na Juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ili kuhifadhi rasilimali Misitu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Halmashauri za Wilaya na wadau mbalimbali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ikiwamo Shirika la Mpingo (MCDI), FORVAC, WWF, TFCG na Mjumita bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya Uharibifu wa Misitu kutokana na matumizi yasiyo endelevu.
Aidha, amewapongeza waandaaji wa Mkutano huo (Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kanda ya kusini na Shirika la Mpingo (MCDI) kwa adhma ya kuwakutanisha Watalaam ili
kujadiliana juu ya namna bora ya kuimarisha Usimamizi wa Misitu katika Kanda ya Kusini.
Alisema, kuna tabia mbaya inayofanywa na Wananchi wanaofyeka Misitu kwa ajili ya kilimo cha kuhamahama, uchomaji moto hovyo, ufugaji ndani ya Misitu ya Hifadhi na uvunaji usiofuata Mpango wa Uvunaji.
Telack amewataka wadau na wataalam kutafuta namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo ili kunusuru rasilimali za Misitu ambayo ni muhimu katika kuchangia pato la Taifa, vyanzo vya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za matumizi yasiyo endelevu ya misitu ikiwamo uchomaji moto ovyo, kilimo cha kuhamahama na kuchunga mifugo ndani ya maeneo ya Hifadhi.
Alisema,kwa sasa sekta ya Misitu inachangia asilimia 3.5% ya pato la Taifa ni dhahiri kuwa sekta ya Misitu ni fursa mojawapo ambayo ikitumika kikamilifu itachangia zaidi katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Lindi, Mikoa yote ya Kanda ya kusini na Taifa kwa ujumla.
Alieleza kuwa,Misitu ina fursa nyingi za Utalii, hivyo ni muhimu kwa wataalam na wadau wa misitu kupanga namna nzuri zaidi ya kuboresha na kuvitangaza vivutio vya Utalii na fursa zingine katika rasilimali Misitu ili kuchangia na kuunga mkono juhudi za Mh. Rais Samia Suluhu Hassan za Kutangaza Utalii kupitia Filamu ya Royal Tour.
“Naomba sana waandaaji, mjiwekee utaratibu wa kufanya vikao hivi mara kwa mara ili kuwa kuwakutanisha Watalaam kutathimini utekelezaji wa yale mliyokubaliana, kupanga nini kifanyike na kukabiliana na mambo yanayojitokeza”alisema Mkuu wa mkoa”
Naye Afisa Uhifadhi Mkuu wa wakala wa huduma za misituTanzania anayeshughulikia masoko na usimamizi wa rasilimali za misitu Salehe Beleko alisema,lengo la mkutano huo kukutanisha wadau wote wa misitu kwa ajili ya kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya misitu kwa kuamini kwamba hakuna sekta inayoweza kusimama pekee yake bila kushirikiana na wadau wengine.
Alisema,TFS ina majukumu mbalimbali ikiwamo kuanzisha na kusimamia misitu ya hifadhi na hifadhi za nyuki za Serikali kuu,kuanzisha na kusimamia mashmba ya miti,kusimamia rasilimali za misitu na nyuki katika ardhi,kusimamia utekelezaji wa sheria,seraza misitu na ufugaji nyuki,kukusanya maduhuli ya serikali,kutoa huduma za ugani(elimu y usimamizi wa misitu) na kufanya biashara ya mazao ya na huduma za misitu na ufugaji.
Alisema, changamoto kubwa katika usimamizi na utekelezaji wa sera na sheria za misitu changamoto kubwa ni uchomaji misitu ovyo wakati wa kiangazi unaosababisha kuungua kwa miti midogo ambayo ni muhimu kwa bioanuai,mahitaji makubwa ya mkaa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na migogoro ya mipaka kati ya vijiji na misitu ya serikali kuu au kati ya misitu ya vijiji na misitu ya Serikali .
Hata hivyo alieleza kuwa,TFS imejipanga kumaliza migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji kwa njia ya mazungumzo na kutengeneza mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji,kutoa elimu ya usimamizi wa misitu na madhara ya moto kwa jamii na kuhamasisha upandaji wa miti inayokuwa haraka kwenye mashamba yao itakayotumika kuvuna kwa ajili ya kutengeneza mkaa na matumizi mengine ya kawaida.
Kwa upande wake Kamanda wa wakala wa huduma za misitu Tanzania kanda ya kusini Kamishina msaidizi Manyise Mpokigwa amewaomba wadau wa misitu kushirikiana na TFS katika kutekeleza na kusimamia rasilimali za misiti na nyuki ili ziwe endelevu na kuchangia uchumi wa nchi yetu.