Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Waziri Kindamba (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano baina wakulima, Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech uliofanyika katika Ofisi ya Halmashauri Wanging’ombe, Njombe.
Wakulima wa Halmashauri ya Wanging’ombe wakiwa kwenye mkutano uliofanyika baina yao, Serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech.
Wakulima wa Wanging’ombe, Watendaji wa Kampuni ya Longping High Tech na ujumbe walioambatana nao wakifurahia jambo walipotembelea kwenye moja ya shamba la soya.
……………………………………………..
Wakulima wa zao la maharage ya soya wa Kanda ya Kusini wamevutiwa na aina ya uwekezaji unaotarajiwa kufanywa na Kampuni ya Longping High Tech ya nchini China, ambayo inalenga kuwawezesha wakulima wa soya katika maeneo mbalimbali nchini kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo.
Haya yamejili wakati wa ziara inayoendelea, kwa Watendaji wakuu wa Longping kutembelea maeneo yanayozalisha maharage ya soya nchini. Mkurugenzi wa Biashara za Nje na Fedha wa Kampuni hiyo Bw. Shangyang Wu akizungumza na wakulima wa Wanging’ombe Mkoani Njombe ameeleza kuwa lengo la Kampuni hiyo kuwekeza nchini kupitia wakulima hao inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mahitaji ya soya kuliko kiasi wanachokizalisha nchini China, kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali ya Tanzania na China ambapo China iliahidi kuisaidia Tanzania kuongeza uzalishaji wa soya nchini na baadae kununua zao hilo kutoka kwa wakulima.
Tumetembelea maeneo mbalimbali na kuonana na kufanya mazungumzo na wakulima, tumeridhishwa na jitihada na nia ya wakulima na serikali katika kuongeza ubora na kiwango cha uzalishaji wa soya. Nitoe ahadi kwenu kuwa tumejipanga na tupo tayari kufanya kazi na wakulima wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ili kutimiza adhima yetu ya kuona maisha ya wakulima yanaboreka kutokana na kipato kinachotokana na maharage ya soya. Tumesikia changamoto zilizopo, tutasaidia kuzitatua ili kuongeza tija kwa mkulima. Alieleza Bw. Shangyang Wu.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Waziri Kindamba kwa upande wake amewahimiza wakulima hao kuchangamkia fursa ya uzalishaji wa soya kwa kushirikiana na kampuni ya Longping kwa kuwa tayari wameshahakikishiwa soko la uhakika la nchini China. Vilevile Mhe. Kindamba aliwaeleza watendaji wa Kampuni ya Longping kuwa Serikali ya Mkoa inataoa ushirikiano wa dhati kwa pande zote mbili (Wananchi na Kampuni ya Longping) ilikuhakisha wote wanafikia matarajio yaliyokusudiwa.
Niwasihi wananchi wenzagu hii sio fursa ya kuipoteza, tujipange kuzalisha soya kwa uwingi na ubora tutakao kubaliana kwa kuwa changamoto yetu ya muda mrefu ya ukosefu wa soko Longping wamelitatua. Niwahikikishie kuwa katika hili Serikali ya Mkoa hatupo tayari kuacha mwananchi yeyote nyuma kufikia maendeleo, tutendelea kuhimiza na kumtaka kila mmoja wetu kufanya kazi kwa bidii ili anufaike na fursa hii ya zao la soya. Alisema Mheshimiwa Kindamba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano baina yao, serikali na Watendaji wa Kampuni ya Longping wakulima wa Wanging’ombe wameeleza kuridhishwa kwao na mkakati wa uwekezaji wa kampuni hiyo. Aidha wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuhakisha wananchi wanapata fursa ya masoko ya mazao wanayoyazalisha. Vilevile wameeleza utayari wao wa kushirikiana na kampuni ya Longpin kwenye uzalishaji na uuzaji wa zao la soya.
Katika hatua nyingine Watendaji wa kampuni ya Longpin wakiwa mjini Iringa walionana na kufanyamazungumzo na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Queen Sendiga. Katika mazungumzo yao walijadili namna wakulima watafikiwa na kunufaika na fursa ya uzalishaji wa soya. Mheshimiwa Sendiga aliwahikikishia wawekezaji hao kuwapa ushirikiano katika hatua zote za uwekezaji katika Mkoa huo.
Longping High Tech ni miongoni mwa Kampuni wa kubwa nchini China inayoongoza katika uzalishaji wa mahindi ya njano, maharage ya soya na mtama. Kampuni hiyo pia imewekeza nchini Brazil kwa Dola za Marekani Bilioni 1. China inahitaji maharage ya soya kiasi cha tani milioni 155 kwa mwaka.
Wakiwa ziarani watendaji wa Longping wamepata fursa ya kutembelea mashamba ya mazao mbalimbali ya wawekezaji, kuzungumza na vikundi vya wakulima na kutembelea wazalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo ikiwemo mahindi na soya. Ziara hiyo inahusisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na Rukwa.
Katika ziara hiyo Watendaji wa Longping wameambatana na watendaji wa Selikali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Kilimo, The Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (“SAGCOT”) na Mkurugenzi wa Longping Tanzania Bw. Joseph Kusaga