**********
Na Mwandishi wetu
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Temeke,Abdallah Mtinika amesema kutokana na utamaduni uliojengeka suala la hedhi limekuwa halizungumziki mara kwa mara katika jamii na kufanya uelewa wa jambo hili kutofahamika kwa mapana yake.
Pia amesema Wadau mbalimbali wa hedhi wanapokutana na kukumbuka kundi la wasichana na kutoa elimu inasaidia jambo hili kuongeza uelewa wa jambo hili ambalo ni kawaida kwa binadamu wakike.
Akizungumza hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi taulo za Kike kwa wasichana wenye ulemavu wa shule ya msingi Jeshi la Wokovu,alisema ni changamoto katika shule nchini juu ya usalama wa watoto hasa wakike wanapokuwa katika siku zao za hedhi.
Alisema suala la hedhi ni jambo la kawaida pale ambapo tendo la uzazi alijakamika inapelekea mwanamke apate hedhi.”Hili ni tukio la kimaumbile la binadamu na wala sio jambo baya sana ni mfumo wa mayai ya uzazi kama yakikosa kurutubishwa basi yanafikia yanatoka,ni suala la kuhakikisha watoto wetu wanakuwa wasafi wanatambua jambo hili kwani sio jambo jipya ,”alisema.
Kwa Upande wake Mratibu wa Taasisi ya Care for Girl with Disabilities,Penina Malundo alisema kundi la watoto wakike wenye ulemavu mara nyingi linakuwa linasahaulika katika jamii,hivyo wameona vyema kuungana kwa kuchangisha fedha kwa watu binafsi pamoja na washirika katika kusaidia kundi hilo.
Alisema taasisi hiyo imeweza kukusanya takribani taulo za kike 300 na kugawa katika shule hiyo pamoja na shule ya msingi mtoni maalum.
“Kama wadau wa kusaidia jamii kwa upande wa watoto wakike hususani wenye ulemavu , tumeona ni vyema siku hii ya kilele cha maadhisho ya siku ya hedhi duniani kujumuika na mabinti wenye ulemavu wa viungo katika Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu na Shule ya Msingi Mtoni Maalum kuhakikisha wanakuwa salama na wenye furaha wakati wote hasa wanapokuwa kwenye mzunguko wao wa hedhi,”alisema na kuongeza
“Mei 28, siku kama ya leo hufahamika kama Siku ya Hedhi Salama Duniani, ikumbukwe kuwa kila mwanamke hupata mzunguko wa hedhi kila mwezi, ambapo utando katika kuta za uterasi huvunjika na kutoka nje ya mwili,”alisema Malundo
Alisema wakati suala la hedhi sio jambo la aibu, lakini bado kuna wanawake hasa wenzetu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana na unyanyapaa na hali ngumu ya kujimudu pindi wanapoingia katika siku zao za hedhi ambao hawezi kujisitiri vyema.
Alisema wanaamini kuwa taulo hizi walizogawa zitawasaidia wasichana hao wenye ulemavu kuwapa ujasiri, kujiamini na kujiona wathamani wanapokuwa kwenye siku zao za mzunguko wa hedhi kwa sababu watakuwa salama.
Mmoja wa watoto hao wa Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu ,Maria Joseph aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwakumbuka na kuomba wadau wengine kuwafikia zaidi katika shule yao.