************************
Na Victor Masangu,Chalinze
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani limejipanga kukabiliana na changamoto mbali mbali ikiwemo wimbi la mianya ya upotevu wa mapato yake ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu wachache.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze mh.Hassan Mwinyokondo amesema kwamba changamoto ya ukusanyaji wa mapato wataivalia njuga usiku na mchana kwa lengo la kuweza kuongeza kasi zaidi katika suala hilo la kuthibiti upotevu wa fedha ya serikali.
Aidha Mwenyekiti huyo alibainisha kwamba watakuwa wakali sana kwa watu ambao wanafanya makusudi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kwamba wataweka mipango madhubuti ambayo itaweza kusaidia kuongeza mapato zaidi.
“Mimi hii changamoto hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa ushuru katika maeneo ya kokoto kwa kweli bado kuna tatizo maana kuna makampuni makubwa tu nayo yanahusika katika ili hivyo inabidi ili Jambo lazima tulifanyie kazi hatuwezi kuona baadhi ya watu wanafumbiwa macho hili Jambo lazima tulivalie njuga,”alisema Mwenyekiti huyo.
Aidha pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo kwa sasa wameshaweka mikakati madhubuti kwa ajili ya kuweza kubuni vyanzo vipya vya matapo ikiwemo mradi wa ujenzi wa soko ambalo litaweza kusaidia kuongeza kiwango cha fedha.
Katika hatua nyingine aliwataka watumishi kuachana na tabia ambazo hazifai na badala yake wahakikishe kwamba wanafanya kazi na kutekeleza majukumu yao ipasavyo bila ya kufanya hujumu yoyote katika miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Diwani Godfrey Kumugisha alisema licha ya juhudi zinazofanywa na serikali lakini bado kuna baadhi ya watumishi na watendaji wanashindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo Kasilda Mgeni ameitaka halmashauri hiyo kuongeza kasi na ubunifu zaidi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato kwani kwa kipindi hiki takwimu zinaonyesha kasi ya ukusanyaji imepungua.
“Kwa kweli Mkuu wa Wilaya ameniagiza niwaambie katika kikao hiki kwamba hajaridhishwa kabisa na ukusanyaji wa mapato kwa sababu ukiangalia kipindi Cha nyuma na miezi hii iliyopita mmeshuka hivyo kunatakiwa kufanyike juhudi za makusudi kuondoa hali hii,”alisema Kasilda.
Kadhalika aliongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo kunahitajika uangalizi wa hali ya juu na kuwahimiza watumishi na wataalamu pamoja na madiwani kuwa na nidhani pindi wanapotekeleza majukumu yao.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Ramadhani Possi ameahidi kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali ambazo zimewasilishwa katika kikao hicho lengo ikiwa ni kuzitafutia ufumbuzi wa haraka na kuwaletea chachu ya maendeleo wananchi.
Katika kikao hicho cha Baraza la madiwani wa halmashauri kimeweza kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali,viongozi wa chama pamoja na wananchi ambapo pia kulifanyika zoezi la utoaji wa zawadi kwa shule za msingi na Sekondari zilizofanya vizuri kwa mwaka 2021.