Baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakisikiliza mada toka kwa watendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA).
Baadhi ya wahariri wa Vyombo vya Habari nchini wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA. Bi Khadija Mwenda
Mkurugenzi wa Usalama na Afya Eng. Alex Ngata toka OSHA akiongea na wahriri wa vyombo vya habari nchini, kwenye kikao kazi kilichofanyika ofisi za OSHA Kinondoni.
Mkurugenzi wa Mafunzo,Utafiti na Takwimu toka OSHA ndugu Joshua Matiko akiwalisha mada kwenye kikao baina ya OSHAna waharirir wa Vyombo vya habari nchini.
Kaimu Mtendaji mkuu wa OSHA Bi. Khadija Mwenda akiongea na wahariri mbalimbali toka Vyombo vya habari nchini.
**********************
Wito umetolewa kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuongeza jitihada katika kusimamia viwango vya usalama na afya katika sehemu za kazi ili kuwezesha utekelezaji wa sera ya serikali ya uchumi wa viwanda kuwa na tija zaidi.
Wito huo umetolewa na Jukwaa la Wahariri (TEF) wakati wa kikao kazi baina yao na menejimenti ya OSHA kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Katibu wa TEF, Nevelle Meena, amesema
OSHA ina wajibu mkubwa katika kulinda afya za wafanyakazi katika sekta ya umma, sekta binafsi pamoja sekta isiyo rasmi hivyo ni muhimu kwa taasisi hiyo kuhakikisha kwamba jamii ina uelewa wa kutosha kuhusu usalama wao wawapo kazini.
“Kikao cha leo kimekuwa ni cha muhimu sana kwani wahariri au waandishi wa
habari ni watu ambao wanakaa katikati ya taasisi fulani iwe ya binafsi au ya umma
au kati ya serikali na wananchi kwaujumla hivyo OSHA wameona kwamba wahariri wanaweza kuelimisha watanzania kuhusu kazi wanazozifanya, manufaa ya kazi wanazozifanya pamoja na faida ya wale wahusika kutekeleza matakwa sheria ya usalama kazini,” alisema meena.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema lengo la kikao hicho
ilikuwa ni kubadilishana uzoefu na kuwafahamisha wahariri kuhusu namna ambavyo OSHA inatekeleza majukumu yake ili kufanikisha suala zima la kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama na afya katika sehemu za kazi.
“Changamoto kubwa inayotukabili kwasasa ni uelewa mdogo kuhusu masuala ya
usalama na afya miongoni mwa wadau wetu na kwakutambua mchango mkubwa wa tasnia ya habari katika kuelimisha umma ndio maana tumeona tuwashirikishe ili wao kwanza wapate elimu ya namna gani sisi tunatekeleza majukumu yetu katika kusimamia nguvu kazi ya taifa na vile vile waweze kujua wanaporipoti masuala ya OSHA basi wanaripoti katika mstakabali gani,” alisema Mwenda.
Manyerere Jacton ambaye ni Naibu Mtendaji Mkuu wa gazeti la Jamhuri alisema:
“Vikao vya namna hii vinatusaidia sana, kwasababu sisi wahariri sio malaika hatujui kila jambo na kama wahabarishaji wakuu wa wananchi ni sharti kwanza tuwe tunayafahamu mambo kwa undani ili zile taarifa tunapokuwa tunazifikisha kule ziwe za uhakika.”
Aliongeza kuwa OSHA ni taasisi kubwa yenye umuhimu wa kipekee katika uhai wa
wafanyakazi wa kitanzania na katika mustakabali mzima wa uchumi wa nchi.
Nae Angela Mang’enya, Mhariri kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC),
alisema kikao hicho kimewafungua mawazo na kuwapa elimu kuhusu namna
ambavyo OSHA inatekeleza majukumu yake na hivyo kuwawezesha kuwaelimisha
zaidi wananchi kuhusu umuhimu wa kujilinda dhidi ya magonjwa na ajali zitokanazo na kazi.
OSHA ni Wakala wa serikali china ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na
wenye Ulemavu) ambao una wajibu wa kuwalinda wafanyakazi dhidi ya magonjwa, ajali na vifo vitokanavyo na kazi kupitia kusajili sehemu za kazi, kuzifanyia ukaguzi na kuhakikisha kwamba mazingira ya kazi yanakuwa salama wakati wote.