Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo akitoa salamu za ujumbe katika ziara yake
Viongozi walioambatana na Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo wakiwafuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa inaendelea katika kikazo kwenye wakati wa ziara hiyo.
Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Uganda.
Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owinyi- Dollo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa menejimenti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
……………………………………..
Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo leo tarehe 25 Mei, 2022 amefanya ziara ya kutembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na kujionea shughuli mbalimbali zinafanywa.
Katika ziara yake, Mhe. Owiny-Dollo ameambatana na Maafisa 12 kutoka nchini Uganda. Miongoni mwa aliombatana nao ni Jaji Kiongozi wa Uganda Mhe. Dkt. Flavian Zeija, Msajili ya Mahakama ya Uganda, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa JTI Uganda, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya JTI Uganda, Msajili waTaasisi ya JTI Uganda na viongozi wa International Development Law Organization Uganda(IDLO).
Akiongea akiwa kwenye ziara hiyo, Mhe. Owiny-Dollo alisema kuwa lengo la ziara yao ni kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa jinsi ya kuwandaa Maafisa Mahakama ambao wamepangiwa majukumu mapya na kujifunza jinsi ya kuijengea uwezo Taasisi ya Mafunzo ya Kimahakama ya nchini Uganda (JTI) pia kujenga ushirikiano katika masuala mbalimbali yanayohusu vyuo na jinsi ya kuiwezesha Mahakama ya Uganda kufanikisha katika maboresho yake kiutendaji.
Mhe. Owiny-Dollo aliendelea kwa kusema kuwa mafunzo ya kuwandaa Maafisa wa Mahakama wanaopewa majukumu mapya ni muhimu katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo huduma bora ya utaoji haki kwa wananchi.
Alisema wanataka kupata uzoefu ambao utawasaidia yeye na ujumbe kutoka Chuo cha Mahakama cha Uganda kuwawezesha watumishi wanaopewa majukumu mapya kupata mafunzo ambayo yatasaidia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Maafisa wa Mahakama walioandaliwa kwa kupewa mafunzo mazuri wataelewa vema majukumu yao na mambo ambayo anatakiwa kufanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kupata haki wanapokuwa na mashauri” alisema
Alipokuwa akiwakaribisha wageni hao, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika alionyesha furaha yake kwa kuushuru ugeni huo kwa kusema kwamba ujio wao ni fursa muhimu ambapo wataitumia kwa kujifunza mambo mbalimbali na kubadilishana uzoefu jinsi vyuo vya Mahakama vinavyofanya kazi.
Naye Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa anaelezea historia ya Chuo kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge, Sheria Namba 3 ya 1998. Kilianza kazi yake tarehe 23 Oktoba, 2000 na kilikuwa kinatoa Cheti na Diploma ya Kozi za Sheria. Uzinduzi rasmi ulifanywa na Rais Benjamin Mkapa tarehe 3 Agosti 2001. Pamoja na historia hiyo Mkuu wa Chuo alieleza lengo la madhumuni ya kuanzishwa kwa Chuo ilikuwa ni kujengea uwezo watumishi wa Mahakama.
Ziara hiyo ni sehemu ya ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uganda na ujirani mwema kati ya nchi hizi mbili. Sambamba na kutembelea maeneo mbalimbali ya Chuo, Wageni hawa wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vilivyopo katika Wilaya ya Lushoto.