Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya madereva bodaboda na bajaji (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi ya Madereva Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Boniface Mbao akitolea maelezo baadhi ya kero ambazo zilitolewa na Madereva wa Bajaji na Bodaboda Mkoa wa Dodoma wakati wa uzinduzi wa Ujenzi wa Ofisi ya Bodaboda Mkoa wa Dodoma
Baadhi ya Madereva wa Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi ya Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma.
………………………………………………….
Na Bolgas Odilo, Dodoma.
MADEREVA wa pikipiki (bodaboda) na bajaji Mkoa wa Dodoma wametakiwa kufuata sheria za barabarani ili kujilinda wao wenyewe pamoja na watumiaji wengine wa barabara dhidi ya ajali za barabarani.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka alipokuwa akizungumza na madereva hao wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi ya madereva bodaboda pamoja na bajaji Mkoani Dodoma.
Mtaka amesema kuwa, kumekuwa na tabia ya madereva wengi wa bajaji na bodaboda kujichukulia sheria mkononi hivyo waache tabia hiyo mara moja kwani kwa kufanya ni kuvunja sheria.
“Muache kujichukulia sheria mkononi yaani inafika mahala mtu anatamani kuchoma chombo cha moto cha mwenzake kwa sababu za makosa ya barabarani tuachane na hiyo tabia.
“Ni marufuku kujichukulia sheria mkononi na hilo jambo mkaelezane hata kwenye vijiwe vyenu kwamba haruhusiwi dereva yeyote kati yenu kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa vyombo vya sheria vipo.
“Ukijichukulia sheria mkononi utakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria, sasa fikiria ukichukuliwa hatua za kisheria kwa kuvunja sheria utaachaje familia yako huku nyuma?,” alisema Mtaka.
Pia Mtaka aliwataka madereva hao kukerwa na vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na baadhi ya madereva wenzao kwa kuhakikisha wanakemea na kutoa taarifa kwa atakayebainika anafanya uhalifu huo.
“Ni lazima tukerwe kwa uhalifu unaofanywa na baadhi ya madereva wenzetu, ukiona kuna tukio la kihalifu limefanywa na dereva bodaboda ikuume na uwe mlinzi kwa mwenzio na utoe taarifa kwa polisi.
“Jeshi la Polisi lipo kwaajili ya kutulinda sisi sote hivyo msiogope kutoa taarifa kwa tukio lolote la kihalifu ili tubaki salama,” alisema Mtaka.
Aidha Afisa Uhamiaji Mrakibu wa Uhamiaji Josephati Bulali amewataka madereva wa pikipiki na bajaji kuacha kutumika kuwahamisha wahamiaji haramu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Kwasasa wimbi la usafirishaji wa wahamiaji haramu umehamia kwenye bodaboda na bajaji kwasababu mna uwezo wa kupita nao sehemu mbalimbali kiurahisi.
“Tushirikiane kwa pamoja kutoa taarifa Jeshi la polisi za watu hao wanaotumika katika kusafirisha wahamiaji hao haramu kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na tararibu, kanuni na sheria za nchi yetu,” alisema Bulali.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Boniface Mbao akijibu moja ya wanazopata madereva hao alisema kuwa, “Jeshi la Polisi litaendelea kutoa maelekezo kwa askari wanaosimamia sheria barabarani ili wasiendelee kuwa kero kwa madereva ili muendelee kufanya kazi yenu vizuri,”.