Wakandarasi wa umeme wakiwa kwenye mafunzo ya kujengewa uelewa wa kutumia mfumo mpya utakaozinduliwa hivi karibuni
Afisa uhusiano huduma kwa wateja kutoka Shirika la umeme (TANESCO) Mkoa wa Mwanza mwenye suruali nyeusi Flaviana Moshi akiwa kwenye picha ya pamoja na wakandarasi wa umeme
Afisa tehama Mkoa wa Mwanza Raymond Matovu akiendelea kutoa elimu kwa wakandarasi wa umeme
**********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Zaidi ya wakandarasi 40 wa kutandaza nyaya za umeme majumbani kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza wamepatiwa mafunzo ya matumizi mapya ya mfumo wa Ni-konekt utakaozinduliwa hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa leo hii Mei 25,2022 na Afisa uhusiano huduma kwa wateja kutoka Shirika la umeme (TANESCO)Mkoa wa Mwanza Flaviana Moshi,wakati wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa matumizi ya mfumo huo
Amesema lengo la mfumo huo ni kuboresha huduma kwa wateja,kumaliza tatizo la vishoka,sanjari na kupunguza gharama za ufuatiliaji wa huduma za umeme.
Moshi amesema kuwa mfumo huo unapatikana kwenye mifumo mbalimbali kupitia simu janja kwa kubonyeza *152*00#.
“Tumekuwa tukipata malalamiko mengi kutoka kwa wateja wetu ikiwemo ya kupokea rushwa ndo tuweze kutoa huduma,hivyo tumeboresha kwa kuwa na mfumo huu ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vishoka”,amesema Moshi
Ameeleza kuwa kwa sasa wanahudumia wateja zaidi ya 100,000 lengo lao ni kuendelea kupeleka huduma kwa wateja kutokana na mji unavyozidi kukua.
Kwa upande wake Afisa tehama Mkoa wa Mwanza ambae alikuwa muwezeshaji katika mafunzo hayo Raymond Matovu, amesema kuwa mfumo huo ni rafiki kwa wakandarasi katika utendaji kazi na zitawajengea uaminifu ukilinganisha na awali ambapo malalamiko ya ucheleweshaji wa huduma yalikuwa ni mengi.
Benjamin Gassomi ni Mkandarasi wa umeme kutoka Kampuni ya GGF Limited amesema kuwa mfumo huo mpya utamsaidia kufanya kazi nyingi kwa ufanisi na kwa muda mchache ukilinganisha na zamani ambapo alikuwa akizunguka muda mrefu kufatilia fomu za wateja.
Nae Sylvester Jumanne, ameeleza kuwa kutokana na mafunzo aliyoyapata juu ya mfumo huo mpya anaamini utasaidia sana kuondokana na kero za ufuatiliaji wa fomu na control namba na itawasaidia wateja wao kupata huduma bila usufumbufu.