Jeshi la Polisi Mkoa kwa kipindi cha kuanzia tarehe 20.05.2022 hadi 23.05.2022 limefanya Misako na Doria na kupata mafanikio ikiwemo kuzuia uhalifu na kukamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali ikiwemo watuhumiwa wa kuvunja nyumba usiku na kuiba, kupatikana na Pombe Moshi @ Gongo na kupatikana na mali za wizi.
KUPATIKANA NA MALI ZA WIZI.
Mnamo tarehe 22.05.2022 majira ya saa 03:30 asubuhi, Jeshi la Polisi lilifanya msako huko katika maeneo mbalimbali ya Mji Mdogo wa Mbalizi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa MESTON MWAKAYAMBA [23] Mkazi wa Mapelele akiwa na mali za wizi ambazo ni:-
- TV Flat Screen mbili aina ya Samsung inchi 24,
- Jiko la Gesi lenye Plate mbili na
- Radio aina ya Aborder Subwoofer.
Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na mara upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
KUPATIKANA NA POMBE YA MOSHI (GONGO).
Mnamo tarehe 21.05.2022 majira ya saa 03:45 usiku, tuliendelea na misako huko Kitongoji cha Kilambo, Kata ya Njisi, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela ambapo tulifanikiwa kumkamata PENINA CLEMENT MAGANGA [36] Mkazi wa kitongoji cha kilambo akiwa na lita 10 za Pombe Haramu ya Moshi (Gongo) ikiwa kwenye chupa 03 za maji safi na kidumu cha lita 5. Mtuhumiwa ni mpigaji/mtengenezaji na muuzaji wa Pombe hiyo haramu.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA WIZI MIFUGO.
Mnamo tarehe 21.05.2022 majira ya saa 05:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko katika Kijiji cha Mogelo, Kata ya Mawindi, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali na kumkamata ELIYA YOHANA [35] Mkazi wa Rujewa kwa tuhuma za wizi wa mifugo baada ya kukutwa na kondoo wawili majike huko maeneo ya machinjio ya Rujewa ambako aliwapeleka kwa ajili ya kuchinja.
Kondoo hao walikuwa na thamani ya Tshs 160,000/= Mtuhumiwa alihojiwa na kukiri kuhusika na tukio la wizi na alieleza kuwa kondoo hao aliiba nyumbani kwa NGAPUNDE MASINGISA siku ya tarehe 20.05.2022. Upelelezi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
KUPATIKANA NA MALI YA WIZI.
Mnamo tarehe 21.05.2022 majira ya saa 03:00 asubuhi, Jeshi la Polisi mkoani hapa lilifanya msako huko maeneo ya Stand ya Rujewa, Kata ya Rujewa, Tarafa ya Rujewa Wilaya ya Mbarali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa EMANUEL JOHN [28] Mkazi wa Sumbawanga akiwa na mali ya wizi Pikipiki yenye namba ya usajili MC 202 CYR aina ya Kinglion yenye rangi nyekundu. Mtuhumiwa alikamatwa baada ya kuonekana mwenye mashaka, mara baada ya kumuhoji nyaraka/kadi ya pikipiki hiyo alishindwa kuitoa na kukiri kuwa hana kadi, na pikipiki hiyo ameinunua Tshs. 350,000/= huko Wilayani Chunya kwa mtu aitwaye anamtambua kwa jina moja la EDWARD. Upelelezi wa shauri hili unaendelea ikiwa ni pamoja na msako wa kumpata mtuhumiwa [muuzaji] kwa hatua zaidi za kisheria.
KUPATIKANA NA POMBE YA MOSHI [GONGO].
Mnamo tarehe 21.05.2022 majira ya saa 03:40 asubuhi, Jeshi la Polisi liliendelea na Misako huko Kijiji cha Fubu, Kata ya Ikama, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela, na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili 1. MADENGE ASUMWISYE MWALUNGWE [35] na AYUBU MASHA MWAISEMBA [30] wote wakazi wa Kijiji cha Lusungo wakiwa na pombe haramu ya moshi (Gongo) lita 100 ndani ya madumu matano ya lita 20 kila moja wakiwa wameyabeba kwenye baiskeli zao.
Aidha Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa mmoja ambaye alikimbia na kutelekeza baikeli yake eneo la tukio.
KUPATIKANA NA POMBE ZILIZOPIGWA MARUFUKU NCHINI.
Mnamo tarehe 20.05.2022 majira ya saa 05:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko maeneo ya Kabwe, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya na kumkamata ABRAHAM MWAKAMBELE [25] Mkazi wa Ilemi akiwa na pombe aina mbalimbali zilizopigwa marufuku nchini ambazo ni:-
- Fighter 30,
- Win 12,
- Ice Dry London Gin chupa 72,
- Jambo Gin chupa 06,
- Zikomo chupa 29,
- A one chupa 01,
- Power 35 na
- Hot short 05.
Mtuhumiwa ni muingizaji na muuzaji wa bidhaa hizo zilizopigwa marufuku nchini. Atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri lake kukamilika.
Imetolewa na:
SACP – Ulrich Matei
Kamanda wa Polisi,
MKOA WA MBEYA.