Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamepatiwa elimu ya uchimbaji salama ili kuepusha ajali zinaozoepukika migodini.
Mkurugenzi wa ukaguzi wa migodi na mazingira wa Tume ya Madini, Henry Mditi ametoa elimu hiyo mji mdogo wa Mirerani kwenye mafunzo ya usalama, utunzaji mazingira na usimamizi wa baruti migodini.
Mditi amesema kupitia mafunzo hayo yaliyohusisha wamiliki wa migodi, mameneja na walipuaji wa baruti, wanatarajia ajali za migodini zitapungua kama siyo kumalizika kabisa.
Amesema wamiliki wa migodi, mameneja na walipuaji baruti wanapaswa kuhakikisha wanahifadhi mahali stahili vifaa vya kulipua baruti ili kuepusha ajali zinaozoepukika.
Amesema katika migodi ya madini ya Tanzanite kwa mwaka jana kulitokea ajali 10 na kusababisha vifo nane kwenye vitalu vya madini hayo.
“Usalama mahali pa kazi ni jambo jema hivyo wachimbaji wa madini ya Tanzanite mnapaswa kuchukua tahadhari wakati mnapofanya kazi zenu,” amesema Mditi.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani (RMO) Fabian Mshai amesema ili kuhakikisha utunzaji mazingira unafanyika migodini wameagiza kila mmiliki apande miti 15 kwenye mgodi wake.
“Pamoja na upandaji miti hiyo pia tumekuwa tukiwasihi wamiliki wa migodi, mameneja na walipuaji baruti migodini kuwa makini katika utunzaji wa vifaa vya milipuko ili kuepusha ajali,” amesema Mshai.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Tareq Kibwe amesema wanaishukuru Tume ya madini kwa kutoa elimu hiyo kwani itawakumbusha wachimbaji kufanya kazi salama katika migodi yao.
Mmoja kati ya walipuaji wa baruti Patanumbe Kaaya amesema kwa muda wa miaka zaidi ya 20 aliyofanya kazi hakuweza kusababisha ajali kutokana na kufuatilia kanuni na taratibu za kazi.