Na Mwandishi wetu, Mirerani
MAMLAKA ya mapato nchini (TRA) Mkoa wa Manyara, imetoa elimu ya kodi kwa wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro ili kuwajengea uwezo wa namna ya kulipia kodi zinazowahusu.
Ofisa wa elimu ya mlipakodi wa TRA Mkoa wa Manyara, Nicodemus Masawe ametoa elimu hiyo kwa wamiliki wa migodi na mameneja wa migodi kwenye ukumbi wa Kazamoyo Inn kwa Diwani Luka.
Massawe amesema wamiliki wa madini au wadau wa madini wasiwe na hofu na TRA wawe wanafika ofisi zao zilizopo mji mdogo wa Mirerani ili kufahamu kanuni na taratibu mambo mbalimbali inayowahusu wachimbaji.
“Msiigope TRA kwani hamna mtu anakabwa shingo, kama kuna jambo tunakaa mezani tunapeana elimu hii mamlaka ya seeikali ya kukusanya mapato msihofie,” amesema.
Amesema hivi sasa mji mdogo wa Mirerani kuna kituo cha kiforoza cha TRA kwa ajili ya kuwarahisishia wafanyabiashara wanaosafirisha madini ya Tanzanite nje ya nchi.
Amesema pia mchimbaji mdogo akiwa na mfadhili ambaye ni mwekezaji wa nje atapoteza sifa ya kuwa mchimbaji mdogo.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Tareq Kibwe amesema wanaishukuru serikali kwa kuwaondolea wachimbaji madini kodi ya malipo kwa mishahara ya wachimbaji kwani wachimbaji hawajaajiriwa.
“Kwa hiyo hiyo kodi ya PAYE ya lipa kadri unavyopata inayokatwa kwenye mishahara haipo tena kwetu wachimbaji na kodi ya mapato inayozuiliwa ya withholding tax ilishaondolewa,” amesema Kibwe.
Amesema wale wamiliki waliokuwa na wasiwasi wa kupelekwa mahakamani kutokana na kutolipa kodi ya lipa kadiri unavyopata inayokatwa kwenye mishahara, wachimbaji wasiwe na hofu kwani haipo tena.